Mkataba wasainiwa kuboresha mazingira ya kazi

12May 2018
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Mkataba wasainiwa kuboresha mazingira ya kazi

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Kazi Duniani (ILO), wamesaini mkataba wa makubaliano wenye lengo la kuboresha mazingira ya  kazi kwa nchi wanachama.

Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Balozi Liberat Mfumukeko.

Mkataba huo (MoU) uliosainiwa jana ofisi za makao makuu ya EAC na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Balozi Liberat Mfumukeko na Mkurugenzi wa ILO, Wellington Chibebe, wa ofisi ya Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine unalenga kushughulikia masuala ya ajira kwa vijana, usalama wa jamii na usawa wa kijinsi na uwezeshaji wa wanawake mahala pa kazi.

Mkataba huu umekuja baada ya mwingine uliosainiwa na taasisi hizo, 2001 na mkataba wa 2002 ambao uliwezesha taasisi hizo kujiendeleza na

kuzindua Mpango wa miaka mitano wa mazingira bora kazini (2010-2015).

Akizungumza baada ya kusaini, Balozi  Mfumukeko, alisema mkataba huo uliopitiwa upya umejikita katika maendeleo ya mpangokazi  wa kuweka usawa sera kuhusu usalama wa kijamii kwa nchi  wanachama.

“Mkataba huu unaruhusu kupanua shughuli za biashara kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuongeza ajira, kuendeleza sera inayotaka wafanyakazi kutoka nchi wanachama kufanya kazi nchi yo yote,” alisema.

Alisema jumuiya hiyo imejikita kushughulikia suala la ukosefu wa ajira kwa vijana kama kipaumbele chake, akisema, vijana waliosoma vizuri na

kuelimika lakini wakawa hawana kazi ni bomu linalosubiri kulipuka.

Alidokeza kuwa nchi wanachama wanashughulikia suala hilo kwa kukifanya kilimo kiwe kivutio kwa vijana kufanya kazi katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ILO nchini, Chibebe, alisema taasisi yake itaendelea kufanya kazi na EAC.

“ILO itasaidiana na EAC kuendeleza na kuimarisha mtangamano wa kikanda na wakati huo huo kuhakikisha vigezo vya mtangamano kama uhuru wa kusafirisha bidhaa na huduma, uhuru wa kufanyakazi katika nchi wanachama,” alisema.