M/kiti atoa siku 7 kukamilisha nyumba za walimu

23May 2020
Jumbe Ismaily
Itigi
Nipashe
M/kiti atoa siku 7 kukamilisha nyumba za walimu

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni, mkoani Singida, ametoa muda wa wiki moja kwa idara ya elimu msingi katika halmashauri hiyo kukamilisha ujenzi wa nyumba mbili za walimu katika shule za msingi Mkajenga na Mahinya.

Ally Minja alitoa agizo hilo wakati wa kufunga mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.

“Tumesisitiza masuala ya matumizi ya fedha ambazo tumeletewa na serikali kwa ajili ya miradi, kwanza miradi ya ujenzi wa umaliziaji wa nyumba mbili za walimu wa shule za msingi Mkajenga pamoja na shule ya msingi Mahinya,”alifafanua Minja.

Vile vile, aliwaagiza madiwani kwenda kupambana kwenye maeneo yao kwa kipindi cha wiki moja, kuahidi kuwasaidia kwa siku moja moja kwenye majengo hayo ili fedha walizopewa wazitumie na kuzimaliza ili waweze kuomba nyingine.

Katika hatua nyingine, halmashauri hiyo imepokea Sh. milioni 200 kwa ajili ya kuboresha kituo cha afya cha Rungwa na wananchi wameanza kujitolea nguvu kazi kwa kuchota maji, kuchota mchanga na ufyatuaji wa matofali.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo shule saba za msingi ndizo zilizopatiwa fedha Sh. milioni 75 na endapo zitatumika kwenye matundu ya vyoo zitapata matundu bora yatakayosaidia afya za watoto kuboreka.

Habari Kubwa