Mkopo wa makazi malipo kwa miaka 20 waandaliwa

21Sep 2019
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Mkopo wa makazi malipo kwa miaka 20 waandaliwa

BENKI ya Biashara ya Afrika (CBA), imeanzisha mkopo wa nyumba na makazi ambao utawawezesha wakopaji kulipa kidogo kidogo kwa kipindi kirefu hata kufikia takribani miaka 20.

Mkuu wa Matangazo ya CBA, Julius Konyani.

Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika jijini Arusha, ya kuwapongeza wateja wake inayofahamika kama siku ya wateja wa benki hiyo, Mkuu wa Matangazo ya CBA, Julius Konyani, alisema wateja wao watapata nafasi ya kupewa mkopo wa nyumba na kuulipa taratibu kwa kiwango cha chini.

"Watu wa kipato cha chini wamekuwa wakitumia miaka mingi kufanikiwa kupata makazi bora kulingana na vipato vyao na wakati mwingine wamejikuta wakijenga uzeeni, hivyo tumeliona hilo, tumeanza kuwakopesha viwanja na nyumba na watalipa taratibu kwa muda mrefu," alisema Konyani

Aliwaambia wateja hao kuwa benki hiyo, inafanyakazi kulingana na mahitaji ya wateja wao kwani wengi wana haja ya kuwa na  makazi bora.

Alisema kila mtu anahitaji nyumba, lakini changamoto yao imekuwa ni vipato na baadhi ya taasisi nyingine za kifedha zimekuwa na masharti magumu ya kuwakopesha watu wenye vipato vya chini ndio sababu ya kuanzisha utaratibu wa kutoa mikopo hii.

Prudence Kaijage, ni mteja wa benki hiyo, alisema suala la kuwa na makazi bora ni ndoto ya kila mwananchi na  Watanzania wengi wanavipato vya chini hivyo ni changamoto zaidi.

Hata hivyo, alisema mkopo huo, utawasaidia kuendeleza vipato vyao kwenye shughuli zingine za maendeleo na makazi yatapatikana kupitia uwekezaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CBA, Gift Shoko, awali akizungumza kwenye hafla hiyo, alisema wametenga siku hiyo kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma wanazozitoa kwa wateja wao na kuchukuwa maoni yao ya uboreshaji wa huduma hiyo.

"Hii ni sehemu ya kuwapongeza wateja wetu, kubadilishana mawazo, kupata maoni ya kitu gani wanataka tuboreshe lakini pia ni sehemu ya kutengeneza matandao wa taasisi yetu kwenye masuala ya kimasoko,"alisema Shoko.

Aidha, Shoko alisema walipata malalamiko kutoka kwa wateja wao, kukopeshwa kiwango kidogo cha mkopo usio na dhamana ambapo mteja binafsi alitakiwa kukopa kiwango kisichozidi Sh.  milioni 50, lakini kwa sasa wataweza kuwakopeshwa hadi Sh. milioni 110.

Aidha alisema benki hiyo, imekuwa na utaratibu wa kuandaa hafla ya kukutana na wateja wake kila mwaka kwa lengo la kuwaeleza maendeleo ya taasisi hiyo na kupata  maoni wapi wafanye marekebisho ya utoaji wa huduma.

Habari Kubwa