Mkurugenzi Benki mikononi Takukuru

07Feb 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mkurugenzi Benki mikononi Takukuru

WAFANYAKAZI 20 akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Magreth Chacha, wamefikishwa kwenye vyombo vya dola vikiwamo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kukosa uadilifu na kuisababishia benki hiyo hasara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Magreth Chacha.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Faida Mohammed Bakar, aliyetaka kujua ni hatua gani za kisheria wamechukuliwa viongozi wa TWB kwa kukosa uadilifu.

“Mheshimiwa Waziri umekiri uadilifu hakuna katika benki hiyo na kwamba mnataka kuteua maofisa mbalimbali waadilifu jambo ambalo limedhihirisha kukosekana kwa uadilifu kwa viongozi. Je, hakuna viongozi waliochukuliwa hatua? Alihoji mbunge huyo.

Aidha alisema katika uanzishaji wa benki hiyo, wabunge wengi walichangia mtaji hususan wanawake, lakini hawajapewa shukrani hata ya kutambulika na kuhoji lini watapatiwa barua ya utambulisho na hisa zao.

Akijibu maswali hayo, Waziri Mwalimu alisema watumishi hao waliokosa uadilifu wamechukuliwa  hatua kuanzia Agosti, mwaka jana.

Alisema watumishi hao wamekosa uaminifu na kusababisha benki kupata hasara. 

“Kuna mambo yamefanyika ya ovyo utakuta kuna Saccos imekopeshwa Sh. bilioni moja wanaifuatilia hiyo Saccos, hazionekani hizo fedha zimeenda kwa nani. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Faida kwamba tunaamini PCCB (Takukuru) na polisi watakamilisha uchunguzi haraka lengo ni watumishi hao waende vyombo vya dola na kuchukuliwa hatua,”alisema waziri huyo.

Mwalimu pia alisema serikali imedhamiria kuhakikisha wanapata fedha ya kukuza mtaji wa benki hiyo.

 “Tumepewa miezi sita na BoT (Benki Kuu Tanzania). Nawahakikishia wabunge kuwa Mkurugenzi mpya tuliyemwajiri amefanya kazi kubwa na ingawa ni Benki ya Wanawake tumemwajiri mwanamume ambaye ndani ya miezi mitano amefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha angalau hesabu za benki zinakaa  vizuri,” aliongeza waziri huyo.

Hata hivyo, alikiri kuwa wanatambua mchango wa wabunge wa Bunge la tisa ambao walinunua hisa kwa ajili ya kukuza mtaji wa benki na kwamba watapewa vyeti vyao vya hisa siku chache zijazo baada ya kukamilisha matakwa ya BoT.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua ni lini benki hiyo itaanzisha tawi lake Zanzibar kwa madhumuni ya kuwapatia huduma za kibenki na mikopo yenye riba nafuu kuwainua kiuchumi wajasiriamali wanawake. 

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, alisema benki hiyo ilianza mwaka 2009 na mpaka sasa imefungua matawi mawili yaliyoko jijini Dar es Salaam  na vituo vya kutolea mikopo na mafunzo 305 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Mwanza, Ruvuma na Dodoma.

Aidha alisema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa, ili kuhakikisha benki inajiendesha kwa ufanisi na kukuza mtaji ikiwamo kufanya mabadiliko kwa kuweka uongozi na watumishi waadilifu.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16, inabainisha kuwa benki hiyo ilitoa mikopo yenye jumla ya Sh. milioni 655 bila kufuata taratibu, ikiwamo kuthibitisha uwapo wa kampuni zilizokopeshwa.

Pia ilibainika kuwa hakuna dhamana iliyowekwa kwa mkopo wa Sh. milioni 200 iliyotolewa.

Kadhalika, ripoti hiyo ya CAG ilisema hakuna ushahidi unaoonesha kuwa uthamini ulifanyika kwa dhamana zilizowekwa dhidi ya mikopo yenye jumla ya Sh. milioni 330 na mikopo ya Sh. milioni 355 ilitolewa kwa wateja ambao muda wa matumizi ya leseni zao za biashara ulikwishamalizika. 

Habari Kubwa