Mkutano wa ukuaji wa biashara wawanufaisha Watanzania

22Apr 2016
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mkutano wa ukuaji wa biashara wawanufaisha Watanzania

WAFANYABIASHARA kutoka Tanzania waliohudhuria mkutano wenye lengo la kuwezesha ukuaji wa shughuli za biashara, wamepata mwanga juu ya hali ya biashara na viwanda na fursa zilizopo.

Dk. Manessah Alagbaoso.

Mkutano huo uliandaliwa na Standard Bank ambayo ni benki mama ya Stanbic Bank Tanzania ulifanyika jijini Nairobi, Kenya na kuwakutanisha wateja wake pamoja na kuwawezesha kupanua wigo na ukuaji wa biashara zao.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shughuli za Biashara za Kibenki wa Benki ya Standard kwa Afrika, Dk. Manessah Alagbaoso, mkutano huo ulikuwa ni wa kwanza kati ya mingi ya namna hiyo yenye lengo la kuwezesha ukuaji wa shughuli za biashara.

"Wateja wa shughuli za kibenki wa Benki ya Standard wapatao 70 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Afrika Kusini waliitumia fursa hiyo kupanua mitandao na wigo wa biashara zao katika mazingira na hali bora zaidi," alisema Alagbaoso.

Mbali na hao, alisema mkutano huo ulioanza Aprili 11 hadi 14, mwaka huu, ulijumuisha pia wataalam wa kada mbalimbali wakiwamo mzungumzaji Carole Kariuki, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Private Sector Alliance (KepSA), Dk. Ndiragu Kibata, Mkuu wa Mikakati wa Tauspce na Mchumi wa Benki ya Standard kwa kanda ya Afrika Mashariki, Jibran Qureishi.

Alisema Standard Bank inakusudia kuwawezesha wateja wake kutambua fursa na huduma wanazoweza kuzifikia na hatimaye waweze kuzioanisha na utaalam unaohitajika huku wakiendelea kufaidika na huduma za kibenki zinazotolewa na Benki ya Standard.

Dk. Alagbaoso alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa Standard Bank ili kuhakikisha kwamba inachangia katika kuongeza thamani shughuli za kibiashara kwa wateja wake.

Alisema mazingira ya kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, yamebadilika na kuwa mazuri kwa kuwapo usimamizi mzuri, sheria rafiki na miundombinu imara na bora inayotoa fursa nzuri kwa wawekezaji waliodhamiria kufanya biashara katika ukanda huo.

Dk. Alagbaoso alisema Benki ya Standard ni kubwa kuliko zote barani Afrika na imepata mafanikio makubwa kwa kujikita vilivyo katika sekta ya kibenki Afrika Mashariki.

Habari Kubwa