Mkuu wa mkoa avunja vyama waendesha Bajaji

08Sep 2016
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Mkuu wa mkoa avunja vyama waendesha Bajaji

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, amevunja vyama viwili vya waendesha pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) mkoani hapa na kuagiza madereva hao kuunda chama kimoja ambacho kitakuwa kinafahamika kimkoa.

Alitoa agizo hilo juzi wakati wa mkutano alioufanya pamoja na madereva hao baada ya kubaini kuwa vyama vilivyopo vinasababisha kutokea kwa mivutano isiyokuwa ya msingi.

Aliwataka waendesha bajaji kufanya uchaguzi wa viongozi baada ya kuunda umoja wa mpya na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika, kusimamia uchaguzi huo na kumpelekea taarifa ya utekelezaji ili madereva hao waweze kutambulika.

"Nawapa wiki mbili kutekeleza agizo hili na kuweka utaratibu mzuri wa kufanya kazi zenu za usafirishaji na itakapofika Oktoba Mosi, mwaka huu nitaanza kuwashughulikia watakao kuwa wanakiuka taratibu."

“Kuna vyama viwili vya waendesha Bajaji hapa, kuna kimoja kinaitwa Jumuia ya Wamiliki na Waendesha Bajaji Mbeya (Juwabambe) na kingine Umoja wa Waendesha Bajaji Mbeya, vyama hivi vimekuwa vikisababisha mivutano ya kimaslahi, kuanzia leo navivunja vyama vyote, nawapa wiki mbili muunde upya chama kimoja na kuchagua viongozi ambao watakuwa wanafahamika kimkoa na uchaguzi huo atakuja kusimamia mkuu wa wilaya,”
alisema Makalla.

Aidha, aliwataka madereva hao kuhakikisha wanatii sheria bila shuruti ili kuepuka kuchukuliwa hatua zitakazowafanya wajione wananyanyaswa na Jeshi la Polisi.

Habari Kubwa