Mkuu wa Wilaya akosoa kampuni za simu

20Mar 2016
Elisante John
Singida
Nipashe Jumapili
Mkuu wa Wilaya akosoa kampuni za simu

MAKAMPUNI yanayojishughulisha na mawasiliano hasa mitandao ya simu hapa nchini, yametakiwa kutumia vyema faida wanayoipata kwa kutekeleza miradi mingi ya kijamii ili kusaidiana na Serikali katika kuwaletea watu wake maendeleo.

Said Amanzi akifafanua jambo.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Said Amanzi, wakati wa uzinduzi wa duka la bidhaa za kampuni ya Tigo Mjini Singida, lengo likiwa ni kusogeza huduma zao karibu zaidi na wananchi.

Amanzi aliitaka Tigo na makampuni mengine ya simu kuangalia upya uwezekano wa kurejesha sehemu ya faida kwa jamii inayohudumiwa, ili kuharakisha maendeleo hapa nchini.

“Makampuni yote ya simu, mmewekeza kiasi kikubwa sana cha fedha, hakuna kitu mnachouza nje, mnakusanya hela za wakulima na wafanyakazi wa Tanzania halafu bado mnapeleka nje," alisema Amanzi.

"Sasa kuweni na huruma, toeni kidogokidogo mnachopata ili kisaidie ujenzi wa taifa hili.”
Naye Mkurugenzi wa Tigo kanda ya kaskazini, George Lugata, alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kufungua maduka zaidi Mkoani Singida ikiwemo Wilaya ya Iramba, Manyoni na maeneo mengine nchini, ili kusogeza bidhaa zake karibu na Wananchi.

Aidha, baadhi ya wakazi wa Singida akiwemo Omari Kijida, Seelemani Saidi na Bora Lemmy, walitumia fursa hiyo kuishuru Tigo na kuiomba kuendelea kushirikiana na jamii katika harakati za maendelo ili kupiga vita umasikini, ambao hivi sasa unachukiwa na Watanzania wengi.

Kwa mujibu wa Lubanga, kampuni hiyo tayari imesaidia miradi ya uchimbaji visima virefu 12, katika maeneo mbalimbali Mkoani Singida.

Habari Kubwa