Mpango aagiza taasisi za serikali kuungwa mfumo ununuzi mtandao

11Jul 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mpango aagiza taasisi za serikali kuungwa mfumo ununuzi mtandao

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha taasisi zote za serikali zinajiunga na Mfumo wa Ununuzi ya Umma kwa njia ya Mtandao (TANePS) ili kudhibiti na kuondoa urasimu uliokuwa ukifanyika kwenye manunuzi.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Dk. Mpango alitoa agizo hilo jana, alipotembelea banda la PPRA lililopo kwenye Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara.

Pia aliitaka PPRA, kuweka muda wa mwisho wa taasisi hizo kujiunga na mfumo huo na kuwataka wazichukulie hatua zile ambazo hazitakuwa zimejiunga katika kipindi watakachoweka.

Alisema ni lazima taasisi zote zinazoanzishwa ambazo zina ununuzi mkubwa kujiunga na mfumo huo.

“Fedha nyingi za serikali zinapotea katika manunuzi (ununuzi) ya (wa) umma hivyo ni lazima chombo hicho kikafanya kazi ili kudhibiti urasimu na upotevu wa fedha hizo," alisema Dk. Mpango.

Serikali inaibiwa fedha nyingi kwenye ununuzi ya umma, hivyo ni wajibu wa PPRA kuzibana taasisi hizo.

“PPRA naomba mzibane taasisi zote za umma tena muanze na zile zenye matumizi makubwa ili zijiunge na mfumo huu wasifanye ununuzi nje ya huo mfumo," alisema Dk. Mpango.

Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Umma PPRA, Bertha Soka, alisema tayari mfumo huo umeshaanza kufanya kazi kwa kuziunga taasisi 100 za umma zinazohusika na ununuzi wa vifaa tiba na dawa.

Alisema PPRA ina mpango mkakati wa miaka mitano ambao utakamilika 2019/20 unaojumuisha na mfumo huo.

“Taasisi hizi 100 zitakuwa katika majaribio kwenye mfumo huu katika kipindi chote cha mwaka wa fedha, hivyo tutaendelea kutekeleza agizo la Waziri," alisema Soka.

Habari Kubwa