Mpango awashukia TRA kubambikia kodi wateja

12Jul 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mpango awashukia TRA kubambikia kodi wateja

SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iwachukulie hatua za kisheria ikiwamo kuwafukuza kazi maofisa wanaobambikia watu kodi.

Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alipotembelea banda la TRA.

Alisema mbali na kufukuzwa, watumishi wasio na maadili ambao wamekuwa wakilalamikiwa mara kadhaa wafikishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka ili iwe fundisho kwa wengine.

Wito huo ulitolewa na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alipotembelea banda la TRA kitengo cha maadili, katika Viwanja vya Maonyesho ya 42 Kimataifa ya Biashara yanayotarajia kumalizika kesho.

Dk. Mpango aliagiza watumishi wote wanaolalamikiwa na wateja kuwa na kauli mbaya na wasiotoza kodi halali wachukuliwe hatua za kisheria.

“Moja ya malalamiko ninayopokea sana kutoka kwa wananchi kwenu nyie TRA ni watumishi kutokuwa na maadili. Nilishafikiria kuwafukuza kazi watumishi wote wa TRA kwa sababu hawana maadili, ili tuajiri wengine wapya na wachache ambao watakuwa waadilifu na wanaofanya kazi kwa maadili," alisema Dk. Mpango.

Mpango pia alihoji sababu za kutochukuliwa hatua za kisheria watumishi wanane kati ya 23 waliokuwa na tuhuma za kukosa maadili katika mamlaka hiyo.

 

“Hawa watumishi wanane mliowafukuza kazi mlipaswa kuwachukulia hatua zaidi badala ya kuwafukuza tu kazi, ili iwe funzo kwa watumishi wengine wanaokosa maadili. Nataka watumishi wa TRA watambue kuwa wanayo dhamana ya kuwatumikia Watanzania na kutoza kodi iliyohalali," alisema Mpango.

 

Alisema lengo kubwa la TRA ni kukusanya kodi stahiki kwa wale wote wanaotakiwa kulipa kodi ili kuisaidia serikali kutimiza lengo lake la kuwaletea wananchi maendeleo kukuza uchumi wa taifa.

“Kama msimamizi wa maadili endelea kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wasiyo na maadili, itakuwa fundisho na TRA itakuwa ya mfano kwa kuwa watumishi wanaowajibika kikamilifu," Dk. Mpango aliiagiza TRA.

 

Kadhalika, alimshauri Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, kuendelea kutoa elimu ya kulipa kodi kuanzia ngazi ya shule za msingi na kueleza faida na mafanikio ili wanapokuwa wakubwa watimize wajibu wao.

“Kitengo cha elimu ya mlipakodi mnajitahidi sana kutoa elimu, hongereni sana ila endeleeni kutumia ngoma na vikundi vya utamaduni kutoa elimu zaidi muwafikie mwanafunzi waliopo shuleni kuanzia shule za msingi watambue wajibu na faida za kulipa kodi," alisema Dk. Mpango.

 

 

 

Habari Kubwa