Mpango wa kufuatilia kero wavuvi wadogo ‘wapikwa’

24Nov 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mpango wa kufuatilia kero wavuvi wadogo ‘wapikwa’

SERIKALI imeandaa mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu na kutatua kero zinazowakabili wavuvi nchini.

Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia mpango huo wa kitaifa jijini hapa, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Emmanuel Bulayi, alisema bado wananchi wengi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi ni maskini.

Alisema hali hiyo haikubaliki na ni kinyume na maelekezo ya sera na miongozo mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ya nchi ikiwamo Sera ya Uvuvi ya Mwaka 2015.

“Tumeona ni vyema wadau wa sekta ya uvuvi kutoka maeneo mbalimbali kukutana kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu nchini,” alisema.

Alibainisha kuwa sekta ya uvuvi inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wavuvi wadogo wapatao 202,053 na zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanategemea shughuli zinazohusiana na uvuvi ikiwamo uchakataji na biashara ya samaki na mazao mengine.

Bulayi alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kutatua kero zinazowakabili wavuvi ikiwamo uandaaji wa mpango huo.

Alisema mwongozo huo umeibua na kutoa njia ambazo zikitumika kikamilifu hali ya kiuchumi na kijamii ya wavuvi wadogo itaboresha kwa kiasi kikubwa, huku rasilimali za uvuvi zikiendelea kuvunwa kwa njia endelevu.

“Usimamizi thabiti wa mwongozo huu unaweza kupelekea kuongezeka kwa ajira, kipato, chakula na lishe na hivyo wavuvi wengi kujikwamua katika umaskini uliopitiliza,” alisema Bulayi.

Alishukuru Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa hiari na kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu katika muktadha wa chakula na kuondoa umaskini.

Aidha, alisema pamoja na mwongozo huo kuwa umepangiliwa vizuri, kama utekelezaji wake hautasimamiwa ipasavyo, hautaweza kutoa tija inayotarajiwa.

Naye Mwakilishi wa FAO, Dk. Oliver Mkumbo, alisema umuhimu wa mpango kazi kwa nchi ya Tanzania uko wazi ukizingatia sekta ya uvuvi inategemewa na watu wengi kwa shughuli mbalimbali za kujipatia kipato na lishe.

“Tunatambua juhudi za serikali, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazotekeleza mpango huu, tunaipongeza serikali na wadau kwa kuona umuhimu wa mpango huu na ni matumaini yangu utasaidia kuleta maendeleo kwa wavuvi na jamii kwa ujumla,” alisema Mkumbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kusimamia mazingira nchini (EMEDO), Elitrudith Lukanga, aliipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na mpango huo na kutoa wito kwa mashirika mengine kuhakikisha wanashiriki vyema katika mchakato wa utekelezaji wa mpango huo.

Habari Kubwa