Mpina aagiza kiwanda kuzalisha mara 3 zaidi

03Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mpina aagiza kiwanda kuzalisha mara 3 zaidi

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amekiagiza Kiwanda cha kuchakata samaki aina ya sangara cha Supreme Pearch Ltd., kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, kuanza kuchakata tani 60 badala ya 17 za sasa katika kipindi cha mwaka mmoja.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

Tamko hilo, limetolewa jana baada ya kusomewa taarifa za changamoto  zinazosababisha uzalishaji wa tani zisizofikia uhitaji wa kiwanda . 

Mpina alisema kwa changamoto hizo jitihada za kuondoa uvuvi haramu na kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi na kuzalisha samaki mabwawani, itasaidia kuongeza kiwango cha tani. 

Aidha, Mpina alisema mbinu hiyo ikitumiwa kwa usahihi kwa mwaka mmoja alioutoa, ongezeko la samaki kwenye Ziwa Victoria, litakuwa la kiwango cha juu.

Alisema, samaki wanaovuliwa kwa makokoro na njia zisizo sahihi huua samaki ndani ya ziwa na matokeo yake viwanda kufungwa kwa ukosefu wa malighafi.

"Kuweni makini na kuondoa uvuvi haramu na kusafirisha samaki kwenda nje, hiyo ndio inafanya mtu kuvua samaki hata wa kiwango cha chini,"alisema Mpina.

Awali akisoma taarifa ya hali ya uzalishaji kwenye kiwanda hicho, Meneja Nurudin Salim, alisema utoroshaji samaki kwenda nchi za Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ndio chanzo kikubwa cha kushusha tani.

Alisema kwa siku kiwanda kilikuwa kikichakata tani 60 kwa siku, lakini kwa sasa kinachakata tani 17 na kufikia hatua ya kutafuta mwekezaji mpya wa kukodisha.

Alisema wamekuwa wakichakata minofu ya samaki na kuipeleka kwenye masoko ya Ulaya, Sweeden, hali inayofanya kupata fedha za kigeni na kuchangia kipato cha manispaa.

Habari Kubwa