Mpina akunwa wavuvi, wafugaji kuwezeshwa

06Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Simiyu
Nipashe
Mpina akunwa wavuvi, wafugaji kuwezeshwa

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameisifu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa jitihada kwa kuchochea uongezekaji wa tija katika uzalishaji na mapato ya Watanzania wanaojiajiri katika sekta mifugo na uvuvi.

Akizungumza katika kikao kazi kilichopitia utekelezaji wa malengo na kuzingatia mafanikio yaliyopatikana tangu kikao cha mwisho kilichofanyika Agosti 10, mwaka huu . Waziri Mpina alisema kuwa TADB imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mabenki washirika kuwakopesha wadau wa sekta ya uvuvi na ufugaji na kwa hiyo kizifanya sekta hizo ziwe na maana kwa Watanzania.

“Ninachukua fursa hii kuipongeza TADB kwa jitihada zake za kuisaidia sekta hizi za mifugo na uvuvi kwa kuwa hivi sasa wadau wa sekta hii wanawezeshwa kwa kupatiwa mikopo ya kuendesha shughuli zao,” alisema Mpina.

Alisema amefarijika kuona sekta kama ya uvuvi ambayo haikupewa kipaumbele siku za nyuma lakini sasa TADB imejitosa na inawakopesha wadau wa sekta hiyo na kusema hilo ni moja ya mambo ya kupongezwa na kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo.

Aidha ameisifu benki hiyo kwa kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa zinazotokana na uvuvi na ufugaji kwa kufufua viwanda vikubwa vya maziwa, kikiwemo kiwanda cha maziwa cha ushirika mkoani Njombe.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, amekieleza kikao hicho kuwa benki hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatoa mikopo kwa waombaji wengi zaidi ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

“Hadi hivi sasa benki yetu imepokea maombi ya zaidi ya Sh. bilioni 85.5. Kati ya hizo, zaidi ya bilioni 27 ndio zimeidhiniswa na benki huku zingine zikiendelea kushughulikiwa alisema.

Aliongeza kuwa Sh. bilioni 27 zilizotolewa kama mikopo, Sh. bilioni 3.425 zimepitia Mfuko wa Dhamana kwa Wavuvi na Wafugaji Wadogo, ambao unawawezesha wafugaji na wavuvi kukopa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

“Fedha hizi tunazowakopesha zinawasaidia sana wavuvi na wafugaji kuendesha shughuli zao. Natoa rai wananchi wajitokeze kwa wingi kwani serikali imedhamiria kuwainua na sisi tupo na tutashirikiana nao kuhakikisha wanahudumiwa ipasavyo na kwa wakati,” aliahidi Justine

Habari Kubwa