Msomi nguli akosoa uchumi wa viwanda

11Mar 2017
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Msomi nguli akosoa uchumi wa viwanda

WAKATI sererikali ikiendelea na mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda nchini, imeelezwa kuwa mkakakati huo hautawezekana bila kuwawezesha wakulima wadogo na kuwahakikishia ardhi badala ya kuwezesha wawekezaji wengi kutoka nje.

Wawekezaji hao wanadaiwa kupewa migodi, sehemu za ranchi za kufugia na mashamba makubwa.

Msomi Maarufu wa Afrika na Duniani, Profesa Samir Amin, amesema nguvu ya uchumi wa Afrika ipo mikononi mwa Afrika na kwamba uchumi wa viwanda unategemea wafanyakazi wavuja jasho, hali zao, mishahara yao na nguvu zao za kufanya maamuzi.

Profesa Amin, aliyasema hayo jana katika kongamano lililowakutanisha wanafunzi, wahadhiri, wahitimu na marafiki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa lengo la kujadili nafasi ya mataifa ya Afrika katika kujenga misingi ya uchumi wake na demokrasia yake kwa changamoto zinazotokana na ubeberu unaotamalaki duniani.

“Kama nchi zetu hazitakuwa na nguvu za kushirikiana na kujitegemea kwanza, tutadharaulika, natutadidimizwa na hao wakubwa na hiyo habari ya kujenga demokrasia na uchumi na viwanda vya kisasa haitawezekana kwa sababu ya udhaifu wetu,” alisema Profesa Amin.

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Chuo na Uhusiano wa Wahitimu wa UDSM, Dk. Bashiru Ally, alisema kwa kushirikiana na Uongozi Institute wamemleta msomi maarufu kwa ajili ya kukutana na wasomi wahitimu kujadili masuala hayo.

Alisema changamoto kubwa ni kuwa tangu nchi za Afrika zimepata uhuru hazijajenga misingi ya kujitawala na kujitegemea ndio sababu ya kuitisha mdahalo huo kwa ajili ya majadiliano.

Alisema mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza na mataifa ya Ulaya bado yamedhibiti mifumo ya kijeshi, kiuchumi, kifedha na mifumo ya kimaamuzi kwa sababu mwenye maamuzi ya jeshi na fedha ndio mwenye misingi ya maamuzi.

“Kwa hiyo ndio sababu kwenye masuala ya kisiasa pia hatuwezi kufanya maamuzi sisi wenyewe na ndio sababu tunaangalia ni kwa namna gani kuwajengea wasomi namna ya kujiamini na viongozi wetu namna ya kuwajibika ili kuingia daraja na maendeleo na kazi ya ukombozi bado ni mbichi,” alisema.

Naye Profesa Mwesiga Baregu, alisema wasomi wote nchini wanatakiwa kuungana kujadili kimfumo namna ya kukuza uchumi wa viwanda.

Alisema pia suala hilo lipewe uzito wa kutosha ili kuwa na mfumo wa viwanda na si tu kuwa na viwanda.

“Mchango wa wasomi hauwezi kuonekana kwa kila mmoja kuzungumza kivyake au kila mmoja kufanya lake, bali kwa kuunganisha nguvu ya pamoja,” alisema Profesa Baregu..

Habari Kubwa