Mtafiti aanika maajabu uji wa ulezi

16Oct 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Mtafiti aanika maajabu uji wa ulezi

MTAFITI wa Mazao ya Nafaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Uyole jijini Mbeya, Dk. Denis Tippe, amebainisha maajabu ya uji wa ulezi katika kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto.

Dk. Tippe aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa juzi kuwa uji wa ulezi una virutubisho na madini mengi, yakiwamo ya zinki, ambavyo vinasaidia kukabiliana na udumavu, hivyo akashauri wananchi kutumia uji huo.

Alisema mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inaongoza kwa uzalishaji wa vyakula, lakini inaongoza kwa udumavu wa watoto kutokana na utamaduni wa wananchi kwenye ulaji ambao hauzingatii chakula bora.

Alisema uji wa ulezi ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo hilo ikiwa wananchi wakiutumia pamoja na vyakula vingine vinavyotokana na ulezi.

“Kwa sasa tupo kwenye maadhimisho ya Wiki ya Lishe Duniani, ukifuatilia takwimu, zinaonyesha mikoa yetu ya Nyanda za Juu Kusini inaongoza kwenye uzalishaji wa chakula, lakini inaongoza kwa tatizo la udumavu na sasa hivi inaonyesha tatizo liko zaidi ya asilimia 40,” alibainisha.

Dk. Tippe alisema mikoa hiyo ni miongoni mwa mikoa ambayo zao la ulezi linastawi vizuri na hivyo akasisitiza hakuna sababu kuendelea kukabiliwa na tatizo la udumavu.

Alisema mbali na vyakula vitokanavyo na ulezi kusaidia kukabiliana na udumavu, pia vinawasaidia watu wanaougua ugonjwa wa kisukari kwa maelezo kuwa ni miongoni mwa vyakula ambavyo mmeng’enyo wake unachukua muda mrefu tofauti na mazao mengine.

Pia, alisema ulezi una madini ya chuma ambayo yanasaidia kuimarisha mifupa na meno na hivyo kusaidia watu kuwa na mifupa imara na kutong’oka meno mapema.

Mkurugenzi wa TARI Kituo cha Uyole, Dk. Tulole Bucheyeki, alisema kwa sasa taasisi hiyo imeanza utaratibu wa kugawa uji wa ulezi kwa watumishi na wageni wote watakaokuwa wanatembelea taasisi hiyo.

Alisema lengo la kuanzisha utaratibu huo ni kutoa hamasa kwa wananchi kutumia uji huo pamoja na vyakula vingine vinavyotokana na ulezi ikiwamo ugali.

Alisema taasisi hiyo imefanya utafiti wenye lengo la kufufua mazao mbalimbali ya asili ambayo yalikuwa yameanza kupotea ukiwamo na ulezi kwa maelezo kuwa mazao hayo yana viini muhimu ambavyo vinasaidia kwenye afya za watu.

“Ukiacha kuwa ulezi ni chakuala lakini pia ni uchumi, ulezi tulioufanyia utafiti kwenye kituo hiki unaweza kumsaidia mtu kupata mpaka Sh. milioni 16 kwa ekari moja, hivyo tunawashauri wananchi waanze kuchangamkia,” alisema Dk. Bucheyeki.

Alisema kwa sasa wanataka kubadili fikra za wananchi kuwa ulezi unalimwa zaidi maeneo yenye ukame ili ulimwe maeneo mengi nchini.

Habari Kubwa