Mufti Mkuu aitabiria mema NMB kwa kujali jamii

20May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mufti Mkuu aitabiria mema NMB kwa kujali jamii

MUFTI Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir, ameitabiria Benki ya NMB kufanikiwa katika kuhudumia jamii kutokana na utamaduni wa kuijali, kuithamini na kuipa kipaumbele chini ya mwamvuli wa kaulimbiu yao ya Karibu Yako.

MUFTI Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir.

Mufti Zubeir alisema hayo wakati akizungumza na waalikwa wa hafla ya benki hiyo ya kufuturisha waumini wa dini ya Kiislamu tangu kuanza kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu 2019.

Hafla hiyo iliyoshirikisha waumini wa Kiislamu, wateja na waalikwa wengine, ilihudhuriwa pia na Sheikh Mkuu wa Mkoa, Alhad Mussa Salum na Meya wa Jiji, Issaya Mwita.

“Niwapongeze kwa uamuzi huu wa NMB kufuturisha waumini wa Kiislamu, hasa ukizingatia mnahudumia makundi mbalimbali wakiwamo Wakristo na wasio na dini. Hii inatoa tafsiri moja tu kuwa NMB inajali makundi na kada mbalimbali za jamii, jambo ambalo litawapa mafanikio.

Alisema walichokifanya benki hiyo ni jambo kubwa, linalojenga uhusiano mkubwa baina ya Waislamu na wasio Waislamu, na kila mmoja kuitazama kama taasisi inayojali makundi yote ya watu na kwa namna hiyo wanazivuta nyoyo za wengi kuona inafanya kazi kwa weledi.

“Mtu akiwa mwema kiasi hicho ama hata taasisi, Mwenyezi Mungu humlipa ama huilipa, hii maana yake ni kuwa kwa utamaduni huu, NMB itapata mafanikio makubwa kutokana na namna mnavyojali makundi mbalimbali ya jamii,” alisema Mufti Zubeir.

Aliitaka benki hiyo kutoacha tamaduni ya kufungamanisha makundi kwa kufuturisha waumini wa Kiislamu na kuutaka uongozi kuufanya utamaduni huo kuwa wa kudumu ili pindi awamu moja ya uongozi inapomaliza muda wake, iache alama kwa jamii.

Awali akimkaribisha Mufti Zubeir, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Albert Jonkergouw, alisema benki yake inajisikia furaha kuungana na Waislamu katika kutimiza moja ya nguzo muhimu za dini yao, huku akiahidi kuwa NMB itaendelea kusapoti na kushirikiana na jamii.

Alisema tukio hilo ni la pili tangu kuanza kwa mfungo wa Ramadhani mwaka huu, baada ya kukutanisha, kufuturisha na kujadiliana kwa ufupi na Waislamu wa Jiji la Tanga na kwamba wamepanga kufuturisha katika miji kadhaa Tanzania Bara na Visiwani.

“Tukio kama hili leo linafanyika mjini Iringa, awali lilifanyika Tanga na sasa tunaelekea Zanzibar (Unguja na Pemba), na pia mikoa ya Mtwara, Mwanza na kwingineko kulingana na ratiba itakavyoturuhusu,” alisema Jonkergouw.

Akijibu wito wa Mufti Zubeir, aliyeomba mwendelezo wa hafla za kufuturisha, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, alisema benki hiyo itaendelea na utaratibu wa kufuturisha waumini wa Kiislamu na kwamba wamefanya hivyo mara nyingi na wataendelea.

Habari Kubwa