Mviwata walalamikia ushuru wa masoko

19May 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mviwata walalamikia ushuru wa masoko

MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), umelalamikia, ushuru wa masoko na tozo za kusafirisha kwa gunia badala ya kutozwa kwa uzito.

Walisema hali hiyo inajenga mazingira shawishi kwa wanunuzi na madalali kuzidisha uzito wa vifungashi zaidi ya kiwango stahiki.

Mratibu wa Mviwata mkoani Manyara, Martin Pius, alisema hayo mjini Babati juzi kwenye warsha ya uboreshaji matumizi ya vipimo na kuzingatia vipimo sahihi vya ujazo na matumizi ya mizani wakati wa kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Pius alisema lengo lao ni kutafuta hatua za pamoja kwenye kuboresha biashara ya mazao ya kilimo kwa kuzingatia vipimo sahihi vya ujazo ili kuongeza tija kwa wakulima, wanunuzi na halmashauri kwa ujumla.

Alisema inatakiwa kuandaa mpango wa pamoja unaotekelezeka kwa ajili ya kuwezesha matumizi ya vipimo katika Wilaya ya Babati na kupashana habari ya maboresho katika sheria ya vipimo, kanuni zake na marekebisho yaliyofanywa.

“Matumizi sahihi ya vipimo ni muhimu sana katika kuhakikisha uwazi na uhakika wa vipimo vinavyotumika, ili wazalishaji, wanunuzi na watumiaji walindwe na serikali ikusanye mapato inayostahili na takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo zipatikane,” alisema.

Alisema tafiti zinaonyesha ukosefu wa uelewa kuhusu vipimo sahihi siyo kwa wakulima au wanunuzi tu bali hata kwa watumishi wa umma ambao wana dhamana kubwa katika kusimamia utekelezaji wake.

Alisema mazoea ya kufanya biashara ya mazao ya kilimo bila kutumia vipimo sahihi yapo kila mahali na kimsingi, biashara ya mazao ya kilimo inayofanyika mashambani hufanywa bila kuhusika kwa wakala wa vipimo.

Kaimu Katibu Tawala wa mkoa, Weransari Munisi, alisema ni vyema kutambua kuwa sio uzito tu wenye shida katika biashara hii, bali hata vipimo vinavyotumika vinatofautiana kutoka eneo moja na jingine.

Alisema warsha hiyo ni ya muhimu kutokana na mkazo unaowekwa na serikali kuzingatia vipimo sahihi vya ujazo ikiwa ni pamoja na matumizi ya mizani wakati wa kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Alisema uuzaji wa mazao mabichi shambani ni kosa na hasara kubwa kwa wakulima kwani hakuna kipimo cha kupima mazao yaliyo shambani, na kumkosesha mkulima mapato makubwa yatakayopatikana na uuzaji wa mazao hayo wakati wa kuvuna na kuuza kwa kutumia vipimo sahihi vya ujazo.