Mviwata yaiangukia serikali viuatilifu

24Mar 2020
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Mviwata yaiangukia serikali viuatilifu

MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima nchini (Mviwata), umeiomba serikali kuingilia kati na kudhibiti uingizwaji holela wa viuatilifu nchini ili kumaliza changamoto ya viuatilifu feki na visivyo na viwango.

waziri wa kilimo, japhet hasunga. picha mtandao

Viuatilifu hivyo feki na visivyo na viwango vinashindwa kuua wadudu waharibifu wa mimea.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini hapa na Mwenyekiti wa Mviwata, Mkoa wa Arusha, Mchungaji John Safari, alipokuwa akizungumza na Nipashe kuhusiana na changamoto ya mazao ya wakulima kuvamia na wadudu.

Alisema kuwa wakulima wengi nchini wamekumbwa na adha kubwa ya mazao yao kushambuliwa na wadudu kiasi cha kukosa mavuno, kutokana na dawa zinazoingizwa nchini kutokuwa na uwezo wa kuua wadudu waharibifu.

“Hivyo tunaiomba serikali kupeleka wataalamu wa kilimo vijijini ili kufanya utafiti wa baadhi ya wadudu wasiosikia dawa na kupata dawa zenye uwezo wa kuuangamiza, lakini watusaidie kudhibiti viuatilifu feki vinavyoingia kinyemela nchini,” alisema.

Alisema changamoto kubwa kwa wakulima jinsi ya kupata dawa za kuua wadudu kwenye mazao yao kwani kwa sasa wadudu wamekuwa sugu, hawasikii dawa na kujikuta wakipata hasara kila mwaka.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, alisema serikali imejipanga kutatua changamoto zote zinazowakabili wakulima, hususani wanachama wa Mviwata ili kuboresha shughuli zao za kilimo.

“Lakini sio kujipanga tu bali hata suala la upatikanaji wa mbolea na pembejeo zingine nalo serikali tunalipa kipaumbele, hivyo msiwe na shaka na serikali yenu,” alisema.

Akizungumzia suala la viuatilifu alisema kumekuwapo na tatizo la uelewa juu ya matumizi ya viuatilifu kwa wakulima, hivyo kuchangia sehemu kubwa ya wadudu kushindwa kuangamia.

Aliwataka maofisa ugani na wataalamu mbalimbali wa kilimo, kuhakikisha wanawatembelea wakulima, na kuwapatia elimu juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu

Habari Kubwa