Mvua yakosesha makazi kaya 79 Na Marco Maduhu, SHINYANGA

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
Mvua yakosesha makazi kaya 79 Na Marco Maduhu, SHINYANGA

BAADHI ya wananchi wa vijiji vya Bushoma na Mishepo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, vijijini, wamekosa makazi kutokana na nyumba zao kuezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali, ambayo ilinyesha kwa muda wa nusu saa.

NYUMBA 66 ZAEZULIWA NA MVUA ILIYOAMBATANA NA UPEPO MKOANI SHINYANGA

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa mbili usiku wakati wananchi hao wakiwa kwenye makazi yao. mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali, ilinyesha na kuezua mapaa kwenye baadhi ya kaya na kuzua taharuki kwa miji hiyo na kukimbilia nje ili kuokoa maisha yao.

Diwani wa Mwantini ambako vijiji hivyo viko, Mjenga Samweli, alisema katika  maafa hayo, hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha isipokuwa nyumba hizo zilezuliwa mapaa na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa sehemu za kuishi na kwamba wanafanya tathimini ili kuona namna ya kuwasaidia kupitia kamati ya maafa.

“Katika kijiji cha Mishepo, nyumba 61 zimeezuliwa mapaa, Bushoma kaya 18 hivyo kufanya vijiji vyote kuwa na kaya 79 ambazo zimeathiriwa na mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha katika tukio hili,” alisema Samweli.

“Baadhi ya kaya zimehifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao, lakini wale ambao nyumba zao hazikuharibika pakubwa ndio tunasaidiana na baadhi ya wananchi kuzirekebisha,” aliongeza.

Mmoja wa waathirika hao, Perpetua Masesa, mkazi wa kijiji cha Mishepo, alisema wakati mvua hiyo ikianza kunyesha kulikuwa na upepo mkali na ghafla walishangaa mabati yakianza kung’oka kisha nyumba kubaki wazi, huku vitu vyao vyote vya ndani vikilowa na kuharibika.

Aliiomba serikali kuwasaidia misaada ikiwamo maturubai na chakula wakati wakikusanya nguvu za kufanya ukarabati wa nyumba zao ambazo mapaa yake yameezuliwa.

Habari Kubwa