Mwanri aagiza wanaotoza nauli za juu kukamatwa

04Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
TABORA
Nipashe
Mwanri aagiza wanaotoza nauli za juu kukamatwa

KAMATI cha Ushauri ya Mkoa wa Tabora (RCC), imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoani humo, kuanza kuwakamata wasafirishaji wanaowatoza abiria nauli ambazo sio halali.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

Tamko hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, kwa niaba ya wajumbe wakati wa kikao cha kuwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Mkoa wa Tabora ya mwaka ujao wa fedha.

Alisema kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa abiria kutozwa nauli zaidi ya iliyoandikwa kwenye mabasi kinyume cha utaratibu.

Mwanri alisema vitendo hivyo havikubaliki na ni uvunjifu wa sheria na kuwaibia wanyonge fedha zao, hivyo aliiagiza Sumatra kuweka mtego ambao utasaidia kuwanasa wasafirishaji wanaoendesha vitendo hivyo.

"Sio lazima msubiri hadi abiria walete malalamiko ...wekeni mtego wa kujifanya mnasafiri mtawapata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria...ni vema abiria alipe nauli halali na apatiwe tiketi ili kuhakikisha hakuna uwepaji wa kodi za serikali," alisema.

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo aliwataka abiria kutokubali kutoa fedha zaidi ya iliyoandikwa ubavuni mwa magari na kama watatozwa zaidi wahakikishe wanapewa tiketi na kuipeleka kwa askari wa usalama barabarani ama Sumatra ili wahusika wachukuliwe hatua.

Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Sikonge, Peter Nzalalila, alisema kuna unyanyasaji wanaofanyiwa abiria wa kutozwa nauli ambayo sio halali na kusema kuwa kutoka Tabora kwenda Sikonge wamekuwa wakitozwa Sh. 4,000 badala ya Sh. 3,100.

Aliongeza kuwa katika njia hiyo hiyo, wanaoishia Tutuo wamekuwa wakitozwa Sh. 4,000 badala ya Sh. 2,300 na  wanaoishia Pangale wanatozwa Sh. 3,000 badala ya Sh. 1,500 iliyoidhinishwa na Sumatra.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tabora (Uyui), Said Ntahondi, alisema tatizo hilo lipo njia zote mkoani humo na kutoa mfano wa gharama ya nauli kutoka Tabora Manispaa hadi Goweko abiria anatakiwa kulipa nauli halali Sh. 3,000, lakini amekuwa akilipa Sh. 4,000.

Aliongeza kwa njia ya kwenda Ulyankulu abiria anatakiwa kulipa Sh. 4,100 na kwenda Chemba Sh. 2,500, lakini katika maeneo hayo yote wamekuwa wakilazimishwa kulipia Sh. 5,000.

Ntahondi alisema katika njia ya kwenda Urambo kutoka Manispaa hadi Ussoke abiria wanatozwa Sh. 4,000 badala ya 2,500 na Sh. 5,000 kwenda Urambo badala ya Sh. 4,100 zilizoidhinishwa na Sumatra.

Kwa upande wa Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Tabora, Nelson Mmari, aliwataka abiria wote wanaotozwa nauli zaidi iliyoandikwa wapeleke tiketi hizo ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria ikiwamo kufutiwa leseni ya usafirishaji.

Alisema abiria hapaswi kulipa nauli nje ya ile iliyotangazwa na Sumatra na msafirishaji anatoza zaidi anashiriki kitendo cha wizi.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley, aliwataka abiria wanaokuwa katika magari ya abiria kutoa taarifa kwa askari wa usalama barabarani pindi wanapokuwa wamezidishiwa nauli ili hatua zichukuliwe ikiwamo kurudishia fedha zao.