Mwekezaji Misri kujenga kiwanda cha mitungi gesi

24Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Mkuranga
Nipashe
Mwekezaji Misri kujenga kiwanda cha mitungi gesi

KAMPUNI ya Supreme Holding kutoka Misri inatarajiwa kuwekeza kiasi Dola za Kimarekani milioni 25 (zaidi ya bilioni 40)
kujenga kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki (kulia), akijadiliana jambo na mwekezaji na Mwenyekiti wa Kampuni ya Supreme Holding kutoka Misri, Dk. Moharram Helal (kushoto), baada ya kufanya mazungumzo kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi Mkuranga, mkoani Pwani mwishoni mwa wiki, (katikati) ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Intergas, Dk. Hatem Ahmed. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya kufanya mazungumzo na mmiliki wa kampuni hiyo, Dk. Moharram Helal, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki, alisema mbali ya kutengeneza mitungi, kampuni hitakuwa inajaza gesi na kurejeleza mitungi ambayo imeshatumika.

“Hatujawahi kuwa na kiwanda cha aina hii hapa nchini kwani mitungi yote inayotumika kujaza gezi imekuwa ikiingizwa kutoka nje ya nchi. Hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania ambayo ina hazina kubwa ya gesi,” alisema Waziri Kairuki.

Kwa mujibu wa Kairuki, kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kutengeneza mitungi 1,000 kwa siku na pia kujaza gesi kwenye mitungi 3,000 kwa siku ambayo itakuwa na ujazo kati ya kilo 15 na kilo 30.

“Mpaka kiwanda kitapokamilika kitaweza kuajiri Watanzania 300 na Wamisri 30,” alisema na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Waziri Kairuki amekiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuhakikisha kinatoa msaada stahiki kwa mwekezaji huyo ikiwamo
kujisajili kwa kituo ili aweze kunufaika na huduma zinatolewa na kituo kwa wawekezaji hapa nchini.

“Ningependa kuwashauri wawekezaji nchini kuwasiliana moja kwa moja TIC ili kujiepusha na urasimu usio wa lazima kutoka kwa watu wa kati. Nitaendelea pia kuwakumbusha wawekezaji kuendelea kujisajili na TIC kwani faida zake ni kubwa sana,” alisema.

Alisema amemwomba pia mwekezaji huyo kufikiria pia kuzalisha mitungi yenye ujazo wa chini zaidi ili watu kima cha chini waweze kunufaika na bidhaa zitakazozalishwa au kutengenezwa na kiwanda hicho.

“Tuna mhitaji sana huyu mwekezaji katika eneo hili la kutengeneza mitungi badala ya kuagiza kutoka nje. Nimemwomba afanye mawasiliano na TIC moja kwa moja anapohitaji msaada badala ya kupitia kwa watu wa kati.

Kairuki alimwakikishia mwekezaji kuwa Tanzania ni sehemu sahihi ya kuwekeza na pia kuna fursa nyingi za uwekezaji na mazingira mazuri na rafiki kwa uwekezaji.

Kwa upande wake Dk. Helal ambaye aliambatana na Meneja Mkuu wa Intergas, Dk. Hatem Ahmed, alimshukuru Waziri Kairuki na kumhakikishia kuwa kiwanda kitakamilika kwa muda baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.

“Tumeamua kuja kuwekeza Tanzania kwani tuna amini uzoefu tulionao katika kutengeneza mitungi ya gesi utasaidia kufanikisha ujenzi wa kiwanda. Tanzania ni nchi nzuri sana kiuwekezaji,” alisema.

Habari Kubwa