Mwenge wa Uhuru kuzindua miradi ya bil. 7/- Hal. Singida

23Sep 2016
Elisante John
Singida
Nipashe
Mwenge wa Uhuru kuzindua miradi ya bil. 7/- Hal. Singida

MWENGE wa Uhuru unatarajiwa kuzindua na kuwekea mawe ya msingi miradi mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni saba katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Elias Tarimo, aliyasema hayo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, George Mbijima, alipoongoza msafara wake kuingia katika manispaa hiyo kwa ajili ya kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo.

Tarimo alisema kuwa miradi hiyo ina uhusiano wa karibu zaidi na jamii, ikiwamo kilimo bora, vikundi vya vijana na miundombinu mbalimbali hasa ujenzi wa Kituo Kikuu kipya cha kisasa cha Mabasi Mjini Singida na barabara yenye urefu wa kilomita 1.8 kwa kiwango cha lami.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Mabasi na ujenzi wa barabara, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, aliitaka jamii kuthamini na kuilinda miradi mbalimbali inayoanzishwa na serikali kwa ajili ya maendeleo yao na taifa.

“Hakikisheni mnakitumia vizuri kituo hiki baada ya ujenzi kukamilika, lindeni miundombinu yake idumu muda mrefu zaidi…kituo hiki kitawaingizia pato kubwa vijana na kinamama watakaoendesha shughuli zao mahali hapa,” alisema.

Aidha, katika hatua nyingine, Mbijima alizitaka halmashauri za wilaya, miji, manispaa na jiji nchini, kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kujenga kizazi kipya kinachojali kazi kwa maendeleo yao na taifa.

Alisema baadhi ya vijana nchini wanashindwa kujikwamua kimaisha baada ya kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, hali inayozilazimu serikali za mitaa katika halmashauri za wilaya kushirikiana nao kwa karibu ili kutokomeza hali hiyo.

Baada ya kugawa vyandarua kwa wananchi wa kijiji cha Ughaugha ‘A,’ Mbijima pia alitoa wito kwa jamii kushirikiana na serikali katika mapambano ya malaria ili kuutokomeza ugonjwa huo hasa kwa watoto na wajawazito hapa nchini.

Mapema akisoma risala juu ya ugonjwa huo, Mratibu wa Malaria, Mazengo Charles, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bravo Lyapembile, alisema malaria bado tishio nchini na inahitajika elimu na ushirikiano zaidi kuutokomeza.

Mwenge wa Uhuru mwaka huu, umezindua na kuweka mawe ya msingi kwa miradi mbalimbali katika Manispaa ya Singida na umeendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida