Mwijage ataka kasi uuzaji malighafi nje idhibitiwe

17Jan 2017
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mwijage ataka kasi uuzaji malighafi nje idhibitiwe

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameiagiza Bodi mpya ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), uhakikisha inadhibiti kasi ya uuzaji wa malighafi nje ya nchi ili kuendana na kasi ya uanzishaji wa viwanda nchini.

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua Bodi Mpya ya Tantrade wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika ofisi zao zilizopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Pia aliigiza bodi hiyo kuhakikisha inatoa elimu ya uanzishwaji wa viwanda kwa wajasiriamali na wafanyabishara wadogo ili kuendana na kasi ya mapinduzi ya viwanda.

"Jambo kubwa ni kushirikiana katika kufanya uamuzi ili kuhakikisha tunafikia lengo la kuwa nchi ya viwanda. Jambo la kwanza ni kuhakikisha tunapunguza kasi ya uuzaji wa malighafi nje ya nchi, bidhaa nyingi zitengenezwe hapa nchini zipelekwe nchi nyingine," alisema.

Kadhalika, aliitaka bodi hiyo kuhakikisha inamaliza kazi zilizokuwa zimeachwa na bodi iliyomaliza muda wake tangu mwaka 2015 kwa muda mfupi uliobaki kabla ya Mei, mwaka huu.

Naye Mwenyekiti Mpya wa Bodi hiyo, Mhandisi Christopher Chiza, aliahidi kuwa bodi hiyo itafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Alisema jambo kubwa itakayofanya bodi hiyo ni kutunza mali za taasisi, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusaidia kubuni fursa mpya za biashara zitakazowezesha kukuza sekta hiyo.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Tantrade, Edwin Rutageruka, alisema mamlaka hiyo inategemea mapato ya maonyesho ya kimataifa ya biashara kama mapato ya ndani kwa asilimia 70 huku asilimia 30 yakitoka Serikali Kuu.

Pia alisema mamlaka hiyo imejipanga kuboresha eneo la viwanja hivyo kwa kujenga majengo ya kisasa kwa ajili ya maonyesho na kutumika kwa biashara baada ya maonyesho kumalizika.

Kadhalika alisema wapo katika hatua za mwisho za kuandaa bonanza siku za Jumamosi na Jumapili kwa kushirikiana na wafanyabishara wakubwa, wadogo na machinga ili kupata fedha za kujiendesha.

Habari Kubwa