Mwinyi aahidi kujenga kiwanda cha mwani

17Sep 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Mwinyi aahidi kujenga kiwanda cha mwani

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi, amewahakikisha wakulima wa mwani kuwajengea kiwanda ili kufaidika na zao hilo iwapo atapata ridhaa ya kuwa Rais wa Zanzibar.

Aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za kuomba nafasi hiyo.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia wakulima wa zao hilo kuwajengea kiwanda kama kilichokuwapo kisiwani Pemba, ili kujiendeleza kimaisha na kujipatia maendeleo.

Alisema pia atawawezesha wakulima wa zao hilo kupata taaluma ya ukulima bora, kilimo hicho ambacho wahusika wengi ni wanawake.

Pia alisema serikali atakayoiongoza, iwapo atachaguliwa, lazima iweke nguvu kubwa kwa zao hilo kwa kuwa ndiyo sehemu inayoajiri watu wengi.

Dk. Mwinyi aliipongeza serikali ya awamu ya saba kwa kazi nzuri iliyofanywa katika utekelezaji wa ilani ya kupeleka huduma mbalimbali kwa wananchi zikiwamo umeme na maji na kuahidi serikali ya awamu ya nane chini ya CCM itamalizia pale palipobakia.

“Unapotaka kujenga uchumi mpya lazima uwe na miundombinu bora ya barabara na majengo ya kisasa ambayo (Rais) Dk. (Ali Mohamed) Shein ameanza nami naahidi nitamalizia,” alissema.

Aidha, alisema atawasaidia watu wanaotaka kujenga viwanda vidogo vya kusarifu matunda ili kuwawezesha watu kupata ajira na soko la bidhaa zao.

Dk. Mwinyi alisema serikali atakayoiongoza itaangalia upya mifumo ya kodi na baadhi ya kodi ambazo ni kero kwa wananchi zitaunganishwa ili wananchi wasipate usumbufu.

Kadhalika, alisema pia serikali atakayoiongoza itawatambua rasmi wafanyabiashara wa bodaboda ili kuwawezesha kutambulika kisheria.

Dk. Mwinyi alisema biashara ya bodaboda ni ajira ambayo inamwezesha mwananchi kupata kipato cha kujiendesha kimaisha, hivyo hakuna sababu ya kutotambulika na kutokuwa katika mfumo rasmi.

 

Habari Kubwa