Mwinyi apewa kongole ujenzi Bandari Pemba

16Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Pemba
Nipashe
Mwinyi apewa kongole ujenzi Bandari Pemba

WAFANYABIASHARA kisiwani Pemba wamemshukuru Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa ahadi ya kujengwa bandari ya kisasa Mkoani Pemba, ambayo itasaidia meli za mizigo kufika moja kwa moja.

Hivi karibuni Dk. Mwinyi alikuwa na ziara ya siku nne kisiwani Pemba, ambapo alitembelea miradi mbalimbali na kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao.

Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa kumchagua kuiongoza Zanzibar, ambapo aliwaahidi kuwatekelezea mambo mbalimbali kuhakikisha nchi inapata maendeleo endelevu.

Wakizungumza na waandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao walisema wamefarijika sana kusikia kauli ya Rais ya kujenga bandari, kwani wanaamini gharama za bidhaa zitapungua kwa kiasi kikubwa.

Walisema bidhaa zinapofika kisiwani Pemba zinakuwa ghali sana, hali ambayo inasababisha wananchi kushindwa kununua na hatimaye kukaa muda mrefu bila kupata wateja.

Walisema ikiwa itajengwa bandari ya kisasa, itasaidia meli za mizigo kuja moja kwa moja kisiwani Pemba, hivyo wanaamini kwamba bei ya bidhaa itashuka na kuwapa wafanyabiashara na wananchi ahuweni.

“Bidhaa tunachukua Dar es Salaam au Unguja, kwa hiyo tunapofika Pemba bei lazima iwe kubwa kwa sababu kila tunapopita tunalipia mzigo na ukiangalia pia tunatakiwa tulipe kodi, hivyo lazima tuongeze bei ili na sisi tujilipe gharama zetu,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Mfanyabiashara wa kanga na madera Chakechake, Mbarouk Mohamed Zahor, alisema kauli ya Dk. Mwinyi kutaka kujenga Bandari Mkoani Pemba ni nzuri na anaifagilia sana, kwani anaamini watapata maendeleo kama walivyo wenzao wa nje ya kisiwa hicho.

“Biashara kwa Pemba muda mwingi ni ngumu, lakini hii inasababishwa na kuwa bei ni kubwa na pia mizigo huchelewa kupatikana, hivyo ikiwa itajengwa bandari ya kisasa na mizigo kuja Pemba, itakuwa ni chachu ya maendeleo yetu,” alisema.

Mfanyabiasha wa nguo za watoto, Maulid Ali Kassim, alisema wamefarijika sana walipomsika Rais kuhusu kutaka kuijenga bandari, kwani ushuru utapungua kwa kiasi fulani ukilinganisha na wanapochukua nje ya Pemba.