Mwisho katazo mifuko ya plastiki leo

08Apr 2021
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwisho katazo mifuko ya plastiki leo

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema leo ni mwisho wa matumizi ya mifuko ya plasitiki, ambayo haikidhi vigezo pamoja na kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aprili 5, mwaka huu NEMC iliwakumbusha watumiaji wa mifuko ya plastiki kwamba, mwisho wa matumizi hayo ni Aprili 8, mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka amesema kama ilivyotangazwa awali na baraza hilo, kuhusu ukomo wa matumizi ya mifuki hiyo, ni vyema jamii ikaanza kutumia vifungashio mbadala.

Mapema, Machi mwaka huu, Dk. Gwamaka akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, alisema hakutaongezwa muda wa kusitisha matumizi ya mifuko hiyo kutokana na awali kuchukuliwa hatua kama hiyo.

Dk. Gwamaka alibainisha kwamba, kwa ambao watakiuka katazo la matumizi ya mifuko hiyo, adhabu yake ni pamoja na faini ya kuanzia Sh. 30,000 hadi 200,000 kutegemeana na kosa.

Pia, alisema kuwa wazalishaji wakubwa wa bidhaa za vifungashio vya plastiki ikiwamo viwanda adhabu ni faini ya Sh. milioni tano hadi Sh. bilioni 10 kutegemeana na aina au ukubwa wa kosa.

Habari Kubwa