Naibu Waziri aagiza matokeo ya utafiti yaandikwe Kiswahili

15Mar 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Naibu Waziri aagiza matokeo ya utafiti yaandikwe Kiswahili

NAIBU Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, ameziagiza taasisi za utafiti wa kilimo nchini, kuandika matokeo yao ya utafiti kwa lugha ya kiswahili ili kuwezesha wakulima wengi wa vijijini, kuzielewa na kuzifanyia kazi.

NAIBU Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, picha mtandao

Akitoa agizo hilo Jijini Arusha jana wakati akizindua Teknolojia ya Kilimo Hifadhi, (CASI), iliyofadhiliwa na serikali ya Australia kupitia kituo cha utafiti Selian kilichoibua teknolojia hiyo, Bashungwa, alisema kilimo hicho kina tija na kinatunza mazingira.

Alisema changamoto kubwa iliyopo nchini ni tabia ya watafiti wengi kupitia taasisi zao kuandika tafiti zao kwenye vitabu kwa lugha ya Kiingereza ambayo wakulima wengi hawaelewi lugha hiyo hasa wa vijijini.

"Sasa naagiza taasisi hizi za utafiti wa kilimo zibadilike anzeni kuweka mikakati ya kubadilisha vitabu vyenu vya tafiti na kuweka katika lugha ya kiswahili ili wakulima wengi wa vijijini waelewe na kuzifanyia kazi," alisema.

Alisema tafiti nyingi nzuri kama hiyo ya teknolojia mpya ya kilimo hifadhi (CASI), lakini imeandikwa kwa kiingereza hivyo ueneaji wake kwa wakulima ni wa polepole.

Aliagiza watafiti hao kuhakikisha wanaeneza teknolojia hiyo kwa njia ya midahalo ya kiswahili na vyombo vya habari kwa kuwapatia elimu waandishi ili nao watumie kalamu zao kueneza kwa wakulima wengi zaidi ya sasa.

Alisema serikali inapongeza kituo cha utafiti Selian na serikali ya Australia iliyofanikisha kupatikana CASI kwa sababu inamwezesha mkulima kutumia eneo dogo kuzalisha mahindi na mazao jamii ya kundekunde pamoja na kupata kipato kizuri chenye tija kwake na kuongeza pato la taifa ambalo kwa sasa kilimo huchangia asilimia 29.1.

Pia aliagiza Taasisi ya Kilimo nchini na Taasisi ya uzalishaji mbegu kukaa pamoja na wadau wa viwanda kama SIDO ili watoe dhana za kusaidia wakulima kupalilia na kuvuna, japo teknolojia hiyo inapunguza upaliliaji na uandaaji mashamba kwa muundo wake wa kuacha masalia shambani ambayo hutoa mbolea baada ya kuoza na kuzuia uotaji magugu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mohmoud Mgimwa, alisema teknolojia hiyo nzuri licha ya kuongeza uzalishaji na kupambana na mabadiliko ya tabia ta nchi, pia inapunguza uharibifu wa mazingira.

"Tunachoomba itangazwe zaidi kwenye vyombo vya habari na serikali iongeze bajeti za watafiti ili wafanye kazi vizuri na kuharakisha kupeleka bungeni rasimu ya maadiliko ya sheria ili tutengeneze sheria yenye tija kwa kulinda wakulima," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Selian, Dk Joseph Ndunguru, endapo teknolojia hiyo itaenea kwa wakulima wengi zaidi itawezesha upatikanaji wa malighafi za viwandani na mazao mengi zaidi ya sasa.