Naibu waziri akunwa mradi wa soko

28Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Naibu waziri akunwa mradi wa soko

HALMASHAURI zote nchini zimetakiwa kujifunza kutekeleza miradi ya kimkakati inayopatiwa ruzuku na serikali, katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwa thamani halisi ya mradi wa soko la kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 17 hadi kukamilika kwake inaonekana.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema hayo juzi alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Soko la Kisasa katika Manispaa ya Morogoro wenye lengo la kuzifanya mamlaka za serikali za mitaa kujitegemea kimapato.

Dk. Kijaji alisema kama kuna halmashauri iliyopewa fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kuwekeana mkataba na serikali na bado inashindwa kufuata makubaliano ya mkataba, ijifunze kutoka Manispaa ya Morogoro.

“Ukilinganisha na miradi mingine ya kimkakati niliyoikagua katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huu ni wa mfano. Ziko halmashauri ambazo zimepewa fedha halafu zinarudi tena kuangalia upya mikataba ambayo walitiliana saini na serikali jambo ambalo linatia shaka.

Tuje tujifunze kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa nini amekwenda na wakati ulio katika mkataba,” alisema Dk. Kijaji.

Alipongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 30 japo walitakiwa kufikia asilimia 40 katika kipindi hiki kutokana na changamoto ya kujaa maji na kuutaka uongozi wa Manispaa hiyo kukamilisha ujenzi ndani ya miezi mitano, ili wafanyabiashara waanze kulitumia soko hilo.

"Mapato ya soko hili yataongezeka kutoka Sh. bilioni moja kwa mwaka hadi Sh. bilioni nne, kwa kuwa idadi ya wafanyabiashara itaongezeka kutoka 400 kwa sasa hadi 900 na huduma zingine kama benki zitatolewa, alisema.

Dk. Kijaji alisema dhamira ya serikali ya kuanzisha miradi ya kimkakati kwa manufaa ya Watanzania itatimia kupitia mradi wa soko la kisasa la Manispaa ya Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, aliishukuru serikali kwa kupeleka mradi huo wilayani kwake kwa kuwa soko lililokuwapo lilijengwa mwaka 1953, hivyo kuwa na miundombinu mibovu iliyosababisha wananchi kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu, hivyo mradi huo si tu utaongeza mapato na kuweka mandhari nzuri, bali pia utaimarisha afya za wananchi.

Naye Meya wa Manispaa ya Morogoro, Paschal Kihanga, alisema waliwaahidi wananchi kusimamia ujenzi wa soko hilo jambo ambalo linatekelezwa kwa juhudi kubwa, hivyo kufikia Septemba, mwaka huu, mradi utakabidhiwa kwa serikali na wafanyabiashara wote walioondolewa kupisha mradi na  wengine watarudi.

Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa halmashauri 17 zilizokidhi vigezo vya kutekeleza miradi 22 ya kimkakati nchini kwa mwaka wa fedha 2018/19. Manispaa hiyo ilipata mradi huo wa soko la kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 17.

Habari Kubwa