Naibu Waziri azifunda taasisi za fedha

07Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Naibu Waziri azifunda taasisi za fedha

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ametoa changamoto kwa taasisi za fedha nchini ikiwamo kuhakikisha zinajipanga kikamilifu kukabiliana na suala la mikopo chechefu.

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, picha na mtandao

Alitoa changamoto hiyo jijini hapa wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya Azania.

Pia alizitaka taasisi hizo kupunguza gharama za uendeshaji, ili ziweze kuwahudumia wateja wake kwa gharama za chini zaidi ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.
 
“Chanzo cha mikopo chefu ni watumishi wasio waadilifu kwenye taasisi hizi na ndio maana naomba sana bodi na menejimenti ziwachukulie hatua sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji kwa sababu sisi kama serikali hatutavumilia uzembe wa aina yoyote katika utekelezaji wa hili,” alisema.
 
Alitolea mfano uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushusha riba kwa benki ya biashara kutoka asilimia 16 hadi asilimia 9, kuwa unalenga kuwapunguzia mzigo wa riba wateja wa benki hizo.
 
Alionyesha kuridhishwa zaidi na namna benki hiyo inavyotoa kipaumbele katika kuboresha sekta ya ujasiriamali mdogo na wa kati hatua aliyotaja kuwa itawasaidia makundi hayo kutoa mchango mkubwa katika sekta mbalimbali, ikiwamo ya viwanda vidogo ambayo ndiyo nia ya serikali ya awamu ya tano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Eliud Sanga, alisema benki hiyo inaenda vizuri kimkakati na kiutendaji na ndio maana mwaka wa kifedha ulioisha Desemba 2017, ilifunga na faida ya Sh. bilioni 1.8 toka kwenye hasara ya Sh. bilioni 6 mwaka uliopita na kutoa gawio la faida kwa wanahisa wake.
 
Ili kufanikisha shughuli za kibenki nchini hasa katika mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda, Sanga alishauri masuala kadhaa ikiwamo kuwekeza nguvu ya elimu katika masuala ya fedha pamoja na vigezo vya kupata mikopo kwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe, alisema kwa sasa benki hiyo ina matawi 19 likiwamo tawi hilo jipya lililopewa jina la Sokoine- Dodoma  ikiwa ni ishara ya benki hiyo kutambua mchango wa Waziri Mkuu wa zamani,  hayati Edward Moringe Sokoine katika ustawi wa taifa kwa ujumla.
 
 “Malengo yetu ya kimkakati kwa sasa ni kukuza mtatandao wa matawi ya benki yetu, angalau matawi matatu kwa mwaka na pia kukuza nafasi yetu ya umiliki wa soko ndani ya miaka mitatu,’’ alisema Itembe.
 

Habari Kubwa