Nchi 35 kushiriki Sabasaba

25Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Nchi 35 kushiriki Sabasaba

NCHI 35 zimethibitisha kushiriki katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba mwaka huu.

SABASABA.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka, nchi zilizothibitisha kushiriki ni Botswana, Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ghana, India, Indonesia na Italia.

Alizitaja nchi nyingine zitakazoshiriki kuwa ni Iran, Japan, Kenya, Korea Kusini, Malaysia, Marekani, Misri, Morocco, Nigeria, Pakistani, Palestina, Poland na Rwanda.

Zingine ni Senegal, Singapore, Syria, Sweden, Thailand, Ufilipino, Uganda, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Umoja wa falme za Kiarabu (UAE) na Uturuki.

Rutageruka alisema mamlaka yake inaendelea kuhamasisha na kuwasiliana na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini kwa kuwa mazingira sasa ni wezeshi na hayana urasimu.

Kwa upande wa washiriki alisema kampuni zimefikia asilimia 93.3, lengo likiwa ni kukamilisha asilimia 100 kwa kuwa Watanzania pia wanahitajika sana kutangaza biashara zao hasa katika kipindi hiki ambacho washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani watakuwapo.

Kaulimbiu ya Maonyesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam mwaka huu ni Usindikaji wa mazao ya kilimo kwa maendeleo endelevu ya viwanda, ambayo inaakisi maono ya serikali ya awamu ya tano ya kukuza kilimo kitakachosaidia maendeleo ya viwanda.

Maonyesho hayo yanatarajia kuanza Juni 28 hadi Julai 13, mwaka huu.

Habari Kubwa