Neema kwa wakulima kukopeshwa zana kilimo

28Sep 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Neema kwa wakulima kukopeshwa zana kilimo

BENKI ya CRDB imeingia makubaliano na kampuni zinazouza zana mbalimbali za kilimo, kwa ajili ya kuanza kuwakopesha wakulima zana hizo na kulipa kidogo kidogo ili kuimarisha sekta ya kilimo nchini na kukuza uchumi wa wananchi na taifa.

Akizungumza juzi wakati wa kuingia makubaliano na kampuni hizo, Meneja Biashara wa CRDB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Feruzi Kolongo, alisema mkopo huo hauhitaji dhamana yoyote isipokuwa mkulima atachangia asilimia 25 pekee ya mkopo.

Alisema asilimia inayobakia 75 itachukuliwa na benki hiyo na kwamba lengo la makubaliano hayo ni kuwarahisishia wakulima upatikanaji wa zana hizo na kuinua kilimo biashara nchini tofauti na ambavyo wakulima wengi wanalima kwa mazoea.

“Wakulima wetu wamezoea kila wakienda benki kukopa wanatakiwa waweke dhamana ya nyumba, mashamba na mali zingine zisizohamishika, sasa huu mkopo ni tofauti maana dhamana yake ni huo mtambo utakaokopa,” alisema Kolongo.

Alisema kwa muda mrefu wakulima walikuwa wanaomba mikopo ya zana za kilimo, lakini ilikuwa vigumu kwa sababu taratibu zilikuwa hazijakaa sawa na kwamba kwa sasa wameweka taratibu vizuri.

Aliwataka wananchi kuchangamkia mkopo huo kwa maelezo kuwa una masharti nafuu na mitambo hiyo itawasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuongeza kipato pamoja na uhakika wa chakula.

Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni zinazouza zana hizo, Elia Rajabu, ambaye ni Ofisa Masoko wa Kampuni ya ETC Agro Tractor, alisema wakulima wengi wasingeweza kununua zana hizo kwa pesa taslimu kutokana na wengi kuwa na uwezo mdogo.

Alisema wakulima wengi huwa wanapata pesa kwa msimu hasa baada ya kuvuna na kuuza mazao yao na kwamba wakati mwingine wote huwa wanafanya kazi ya kutumia pesa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kilimo.

“Huu ubia utasaidia wakulima wetu kupata tija kwenye kilimo, tunaamini kuwa huu ni mkopo sahihi kutokana na aina ya dhamana ambayo inatumika ambayo ni zana yenyewe atakayokopa mkulima,” alisema Rajabu.

Baadhi ya wakulima walioshiriki kwenye uzinduzi wa makubaliano hayo, walisema mikopo hiyo imeanza kutolewa kwa muda mwafaka kwa maelezo kuwa miezi hii ndiyo wanayoingia kwenye shughuli za kilimo kwa msimu wa 2020/2021.

Mmoja wa wakulima hao, Amir Mizar, alisema awali matrekta makubwa walikuwa wanatakiwa kulipa Sh. milioni 25, lakini kwa sasa watakuwa wanalipia Sh. milioni 15 ambazo alidai ni rahisi kulipa.

Alisema wakulima wengi huwa wanashindwa kupata tija kwenye kilimo kutokana na kutumia zana duni za kilimo yakiwamo majembe ya mkono pamoja na kupanda mazao kwa kutumia mikono badala ya mashine za kisasa.

Mizar alisema kwa sasa kutokana na uwepo wa mikopo hiyo wakulima wengi watahamasika kuingia kwenye kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao tofauti na ilivyokuwa mwanzo.