Neema kwa wakulima wa karanga mti

04Dec 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Neema kwa wakulima wa karanga mti

ZAO la ‘macadamia’ au karanga mti linalotajwa kulishika soko la dunia kutokana na tunda lake kuzalisha virutubisho muhimu vinavyoondoa uwezekano wa mtu kupata saratani,-

ZAO la ‘macadamia’.

Limegeuka kimbilio katika sekta ya kilimo, baada ya Kampuni ya Namuai Farms Ltd., kutangaza neema ya kiuchumi kwa wakulima wadogo kwa kuahidi kujenga kiwanda cha kwanza Tanzania.

Neema hiyo ilitangazwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Namuai Farms Ltd., Hussein Gonga, wakati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na jopo la wataalamu walipotembelea na kukagua mradi huo mkubwa wa uwekezaji wa sekta ya kilimo.

“Katika kuunga mkono sera ya Rais John Magufuli ya ujenzi wa viwanda ili kuifikisha nchi yetu katika uchumi wa kati, tunatarajia kujenga kiwanda chetu wenyewe cha ku-process (kusindika) mazao ya macadamia tutakayokuwa tukivuna, kutengeneza ajira na kuinua kipato cha wakulima wa nje,” alisema Gonga.

Masoko makubwa ya zao hilo linalotokana na kilimo hai ni nchi zilizopo katika Falme za Kiarabu, Marekani, Ulaya na nchi za Scandinavia.

Mwekezaji huyo mzawa anayemiliki shamba la Namuai lenye ukubwa wa hekari 2,410, ameshapanda miti ya macadamia 23,100 kwenye ekari 165 na kwamba lengo la kampuni hiyo ni kumiliki miti 37,000 katika muda wa miaka mitano ili kuipiku nchi ya Kenya katika uzalishaji huo kwa nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza baada ya kukagua uwekezaji huo, Mghwira, alisema uwekezaji huo utaleta mabadiliko makubwa kiuchumi, kwa kuwa kiwanda kitakachojengwa na mwekezaji huyo kitatumia malighafi zilizopo ndani ya mkoa na pia kitailetea Tanzania fedha za kigeni kutokana na uuzaji wa bidhaa zake katika masoko ya kimataifa.

Mghwira alisema: “Hiki ndio kitu ambacho serikali ya awamu ya tano inakitaka kwamba uzalishaji wa bidhaa uendane na mahitaji ya soko, bidhaa na mitaji izalishwe kukidhi viwanda vinavyotarajiwa kuanzishwa.

 

Zaidi ya watu 20,000 watanufaika na ajira mpya, baada ya kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa viwanda vitano vinavyojengwa na wawekezaji kwa ajili ya kuunga mkono sera ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.”

Mtaalamu wa tiba, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkurugenzi wa Shirika la Better Health Care, Prof. John Shao ameuelezea mmea huo namna unavyotajwa kusaidia afya, kurekebisha sukari, kusaidia kupunguza uzito wa mwili, kuimarisha mifupa, afya ya akili, kusaidia matibabu ya ugonjwa wa Anemia, kuondoa msongo wa mawazo na kutengeneza virutubisho vinavyompunguzia mtu uwezekano wa kupata saratani.

Aidha, Takwimu za Kitengo cha Rejesta ya Kansa ya Mkoa wa Kilimanjaro, inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2013 hadi mwanzoni mwa mwaka 2016, Hospitali ya Rufani ya KCMC ilikuwa imegundua wagonjwa zaidi ya 2,500 wanaougua saratani.

 

Habari Kubwa