Neema malipo makandarasi

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Neema malipo makandarasi

SERIKALI imetangaza kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi huu, itakuwa imelipa Sh. bilioni 609 kati ya Sh. bilioni 962 inazodaiwa na makandarasi waliotekeleza miradi yake mbalimbali.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana jioni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alipohitimisha mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri huyo alibainisha kuwa hadi Juni mwaka jana, serikali ilikuwa inadaiwa na makandarasi Sh. bilioni 833 ambazo haikuzilipa hivyo kuvuka na kuingia katika mwaka huu wa fedha.

"Katika mwaka huu, makandarasi waliendelea kutekeleza miradi na kuzalisha madeni mapya. Hadi Machi mwaka 2019, madeni yalifikia Sh. bilioni 962.

"Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Wizara ya Fedha itakuwa imelipa Sh. bilioni 609 kwa makandarasi mwezi huu," Waziri Kamwelwe aliahidi.

Waziri huyo pia alifafanua kuhusu deni la wafanyakazi wa reli ya Tazara, akieleza kuwa limefikia Sh. bilioni 434, lakini akasisitiza kuwa deni hilo linapaswa kulipwa na nchi mbili; Tanzania na Zambia.

"Lakini katika deni hilo, ikumbukwe kwamba Sh. bilioni 237 ni itifaki ya Serikali ya China ambayo pia inahusisha nchi mbili za Tanzania na Zambia," alisema.

Habari Kubwa