Neema yaja kwa wakulima wa pamba 

09Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Neema yaja kwa wakulima wa pamba 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali imeweka mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote inayolimwa nchini kununuliwa na tayari imeshaanza mchakato wa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) wakati wa kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu. Ndassa alitaka kujua serikali imejipangaje kuwasaidia wananchi walioitikia wito wa kulima pamba iwapo wanunuzi watashindwa kununua pamba yote. Mbunge huyo ameongeza kuwa mwaka jana, Waziri Mkuu aliwaita viongozi wa mikoa inayozalisha pamba na kuwapa maelekezo ya kwenda kufufua zao hilo na wakulima waliitikia wito na mwaka huu wanatarajia kupata mavuno mengi. Waziri Mkuu alisema ni kweli kuwa mwishoni mwa mwaka jana, serikali iliwaita viongozi hao ambao ni wakuu wa mikoa, wakurugenzi na wakuu wa wilaya ambao walipewa maelekezo ya kwenda kuhamasisha kilimo cha pamba  na kuwasaidia wakulima kuanzia ngazi ya awali. Alisema serikali inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa kulima kitaalamu, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko. “Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa hiyo kati ya Februari 15 na 17, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua ili mradi wanajihusisha na pamba,” alisema. Ili kupata uhakika wa masoko nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) inawasiliana na mataifa mbalimbali kuhakikisha pamba yote iliyolimwa nchini inanunuliwa. “Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua ikiwamo pamba. Mengine ni korosho, kahawa, chai na tumbaku, yote kwa pamoja yanachangia kukuza uchumi,” alisema. Alisema awali wakulima wa mazao makuu matano ya biashara nchini likiwamo la pamba, walipunguza uzalishaji baada ya kukosa usimamizi hali iliyoilazimu serikali ichukue uamuzi wa kuyafufua kwa kuwa historia inaonyesha kwamba mazao hayo yanachangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akijibu swali kuhusu ukosefu wa dawa za kuulia wadudu ambalo Ndassa alilalamikia, Waziri Mkuu alisema serikali imeendelea kuagiza dawa hizo kwa kuwa ni sehemu ya mahitaji ya kilimo cha zao la pamba. “Wiki iliyopita niliona kwenye habari Mkurugenzi (Mkuu) wa Bodi ya Pamba akipokea zaidi chupa zaidi za milioni moja na akasema kuna dawa zingine zaidi ya chupa milioni mbili zinakuja. “Ni jukumu la bodi hiyo kuhakikisha dawa za pamba, ziwe za maji au za kupulizia zinapatikana nchini na zinapelekwa kwa wakulima,” alisisitiza.  

Habari Kubwa