Neema yawanukia wakulima mahindi

09Dec 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Neema yawanukia wakulima mahindi

WAKULIMA wa mahindi wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wameanza kupata matumaini ya kuwa na soko la uhakika la mazao yao kutokana na kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao hilo cha East Africa Starch kuwa mbioni kukamilika.

Kiwanda hicho kinatokana na kubadili matumizi ya kilichokuwa kiwanda cha Nguo cha Mbeya (Mbeya Textile) kilichoko eneo la Songwe viwandani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Ofisa Utumishi wa Kiwanda hicho, Mariam Bakari, alisema jana kuwa kiwanda hicho kitakuwa kinazalisha mafuta ya kupikia yatokanayo na mahindi, chakula cha mifugo, glukozi na wanga kwa ajili ya matumizi ya binadamu na viwanda.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata mahindi mpaka tani 90,000 kwa mwaka hali ambayo itawasaidia wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao.

Bakari alisema kiwanda hicho kitakuwa kikubwa kuliko viwanda vyote vya Afrika Mashariki vinavyozalisha bidhaa zitokanazo na mahindi.

“Mbali na kuwahakikishia wakulima uhakika wa soko, pia kitasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuajiri mpaka watu 300 kwa kuanzia na wataongezeka kadri mahitaji yatakavyokuwa yanaongozeka,” alisema.

Mwakilishi wa Kampuni ya Export Trading Group (ETG) ambayo ni miongoni mwa wamiliki wenza, James Mariki, alisema kiwanda hicho kilianza kujengwa mwaka 2017 baada ya kubadili matumizi ya kiwanda hicho ambacho kilikuwa cha nguo.

Alisema kiwanda hicho awali kilikuwa kikizalisha nguo, lakini wakakibadili matumizi baada ya kuadimika kwa malighafi kutokana na serikali kuzuia uzalishaji wa pamba katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa sababu ya kusambaa kwa funza wekundu.

Mariki alisema kwa sasa kiwanda kinachelewa kukamilika kutokana na mgogoro kati yao na makandarasi ambao wanashindwa kukamilisha mradi na baadhi yao wanataka kurejea kwao India kabla ya kukamilisha kazi.

“Kwa sasa serikali imeanza kutusaidia kuwahimiza makandarasi hawa kukamilisha kazi kwa wakati. Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama alikuja hapa na akatoa maagizo kwa makandarasi hawa na sasa tunaamini watakamilisha,” alisema.

Mwishoni mwa mwezi uliopita kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ilifanya ziara kiwandani hapo kwa ajili ya kuangalia maendeleo na kubaini kuwa kiwanda kinachelewa kuanza kazi kwa sababu ya mgogoro uliopo.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, aliiagiza Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, kushikilia hati za kusafiria za mafundi wanaounganisha mitambo ya kiwanda mpaka watakapomaliza kazi hiyo.

Novemba 28, mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim alitembelea kiwanda hicho na kumwagiza Homera kuendelea kushikilia hati za kusafiria za mafundi hao mpaka serikali itakapojiridhisha kuwa kiwanda kinaanza kufanya kazi.

Habari Kubwa