NFRA sasa yaanza kusafirisha mahindi

11Feb 2019
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
NFRA sasa yaanza kusafirisha mahindi

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza kusafirisha mahindi kwenda nchi zenye njaa tani 36,000 ikiwa ni sehemu ya mkataba baina yake na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP).

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankumba, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usafirishaji huo.

Zikankumba alisema kuwa wameshasafirisha mahindi takribani tani 15,000 kwenda katika Uganda na Sudani Kusini.

Alisema mkataba huo ambao uliingiwa kati ya NFRA na WFP ambao pia ulishuhudiwa na Rais John Magufuli, na katika awamu ya kwanza ya mkataba watasafirisha tani 36,000.

"Tumeshasafirisha nusu ya mkataba wetu unaotutaka kusafirisha mahindi tani 36,000, ambapo hadi hivi sasa kama mnavyoona hapa shughuli zinaendelea na tumesafirisha nusu ya mkataba ambapo tani 15,000 zishakwenda nje ya nchi," alisema Zikankumba.

Aidha, aliwataka wakulima kutumia fursa hiyo ya NFRA, kuuza mahindi nje ya nchi ili kulima kwa wingi na kuzingatia ubora.

“Kiasi hiki tunachokiuza sasa hivi tunakitoa kwenye hifadhi yetu, hivyo basi tutatakiwa kuingiza mahindi mengine kutoka kwa wakulima, hivyo ni fursa kwao wakulima kuhakikisha kuwa wanalima mahindi ya kutosha na kuyauza hapa NFRA,” alisema.

Naye, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Dodoma, Felix Ndunguru, alisema usafirishaji huo unaendelea vizuri na wanatarajia watakamilisha kwa muda mfupi. Mahindi hayo ambayo yanasafirishwa kwenda Uganda kutoka Kanda ya Dodoma yanakusanywa kutoka katika kanda saba nchini.

"Hapa Dodoma ni kama sehemu ya kuondokea tunayatoa katika kanda zetu saba za NFRA nchini, ambazo ni Kanda ya Dar es Salaam, Songea, Makambako, Shinyanga, Arusha na Dodoma,” alisema.

Habari Kubwa