NFRA wataka ufanisi usimamiaji maslahi wafanyakazi

23May 2020
Mathias Canal
Morogoro
Nipashe
NFRA wataka ufanisi usimamiaji maslahi wafanyakazi

BARAZA la Wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), wametaka ufanisi kazini kusimamia maslahi ya wafanyakazi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa:PICHA NA MTANDAO

Katika mkutano huo wa siku mbili wafanyakazi wametoa maoni kuhusu umuhimu wa kushirikishwa kwenye shughuli mbalimbali mara kwa mara ili kutambua majukumu yanayofanywa na taasisi hiyo.

Kadhalika, wameomba kuendelea kujengewa misingi ya uwajibikaji hasa katika kutambua wajibu wao kwa umma na kusisitiza kuwa watatekeleza majukumu yao bila uzembe.

Akizindua Baraza hilo juzi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Kilimo, Hilda Kinanga wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, alisema si vema watumishi wakatumia muda mwingi kufanya shughuli ambazo hazina tija zinazoathiri utendaji kazi.

Aliongeza kuwa serikali inayo dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma na hivyo mtumishi anaruhusiwa kudai haki zile za msingi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma wakati wa kutekeleza wajibu wake wa msingi kwa mwajiri na kwa kutumia lugha ya staha.

Wajumbe pia wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu wakala na miongoni mwa ajenda hizo ni kupitia Mpango wa Biashara wa mwaka 2020/2021 (Business Plan), taarifa ya utekelezaji ya robo ya tatu ya mwaka 2019/2020 na kupitia Rasimu ya Miundo mipya ya Maendeleo ya Utumishi.

Katika agenda zilizojadiliwa ya kwanza imewapitisha katika malengo/mipango ya wakala, ya pili ni utekelezaji wa majukumu ya wakala uliofanyika kwa mwaka uliopo na tatu ni mpango wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa lengo ya kuandaa majukumu mapya yanayoendana na muundo mpya wa taasisi.

Kwa nyakati tofauti katika michango yao wamesisitiza kuwa hakuna haki bila wajibu hivyo wana wajibu muhimu wa kutekeleza majukumu yao na ari kubwa.

“Kwa kutambua uzito na umuhimu wa majukumu hayo, kila mmoja katika sehemu yake ya kazi anatakiwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili kuiwezesha serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa wananchi kwa kuwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati,” alikaririwa Meneja NFRA Kanda ya Sumbawanga, Abdillah Nyangasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa, alisema kuwa bado Taasisi ina changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu ya kutoa huduma kwa umma ikiwamo ukosefu wa rasilimali fedha na rasilimali watu wa kutosha, hali inayosababisha kutofikiwa kwa malengo.

Aliwahakikishia kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto hizo ikiwamo kuiomba iwapatie watumishi ili kukidhi matakwa yao.

Alisisitiza watumishi wote wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili katika utumishi wa umma.

Pia, serikali haitasita kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na vitendo vinavyokiuka maadili ya utumishi wa umma.

Habari Kubwa