Ng’ombe 6,600 kutoka Uganda wataifishwa

03Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ng’ombe 6,600 kutoka Uganda wataifishwa

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameendeleza kasi ya kutaifisha mifugo inayoingizwa kutoka nje bila kufuata utaratibu baada ya kuagiza zaidi ya ng’ombe 6,600 walioingizwa kutoka Uganda kupigwa mnada.

Hatua hiyo imefanyika ikiwa ni takribani wiki moja tangu ng’ombe walioingizwa kutoka Kenya kukamatwa na kuuzwa kwa njia ya mnada wilayani Mwanga, Kilimanjaro.

Mpina juzi aliagiza kukamilishwa kwa taratibu za uhamiaji na mahakama kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wilaya ya Misenyi, ili upigwe mnada ng’ombe 6,648 walioingia nchini kinyemela kutoka nchi jirani ya Uganda na kukamatwa.

Alisema uvamizi wa kundi kubwa kama hilo la wanyama linaweza kusababisha madhara makubwa katika mazingira kama vile mmomonyoko wa ardhi, kuharibifu wa vyanzo vya maji, kumaliza malisho ya mifugo iliyoko nchini, kusababisha migogoro ya mara kwa mara kwa wakulima na wafugaji na hata kuleta maambukizi ya magonjwa ya wanyama.

“Sisi serikali hatuwezi kuruhusu hali hii iendelee na mimi nikiwa Waziri mwenye dhamana, nina jukumu la kuhakikisha tunalinda rasilimali hii ya malisho,” alisema.

Mpina alisema suala hilo haliingiliani na ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa ushirika huo upo kisheria, hivyo wavamizi wanaoingiza mifugo kinyemela nchini toka nchi jirani ni wahalifu kama wahalifu wengine.

“Kwa hiyo naangiza ng’ombe hawa 6,648 waliokamatwa hatua ziendelee na ambao hawajakamatwa wakamatwe na wataifishwe na serikali,” alisisitiza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Dennis Mwila, alisema kazi ya kutathmini ng’ombe katika wilaya yake bado inaendelea na taratibu za kisheria zinafuatwa.

Katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Kagera, Mpina jana alitembelea mabwawa ya mradi wa samaki yaliyoko wilayani Muleba katika kijiji cha Luhanga na kusema Serikali ina nia ya kukomesha kabisa uvuvi haramu pamoja na kuwasaka wavuvi haramu waliko.

Aidha, akiwa Bukoba mjini, Waziri Mpina alitembelea kiwanda cha kuchakata samaki cha Suprime Fish Ltd na kuagiza wamiliki wa viwanda vya samaki nchini kuhakikisha wanachukua hatua za haraka kufufua viwanda hivyo na kuongeza uzalishaji kwa kuwa serikali imeshaanza kuchukua hatua kuhakikisha samaki wanapatikana kwa wingi nchini.

Habari Kubwa