Nguvu kuongezwa utalii wa fukwe

12Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Nguvu kuongezwa utalii wa fukwe

TANZANIA inatarajia kuongeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa kuanzisha safari za meli za kisasa katika bahari pamoja na kuanzisha utalii wa mikutano.

Mkakati huo ulibainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda, alipotembelea  maonyesho ya pili ya utalii ya Karibu Kili-Fair yaliyomalizika jijini hapa hivi karibuni.

Alisema hali halisi inaonyesha kwamba utalii wa fukwe una nafasi kubwa ya kuinua uchumi kwa kuwa mara nyingi wageni wanaotembelea huwa na mazoea ya kurudi mara kwa mara tofauti na utalii mwingine wa kutembelea mbuga za wanyamapori.

Alisema baadhi ya nchi zimeanza kutumia utalii wa meli kwa ajili ya vivutio ambavyo vipo katika fukwe, hivyo kuongeza idadi ya watalii na pia kukuza mapato.

Alisema licha ya kuongeza nguvu katika utalii wa fukwe, pia serikali itaongeza aina nyingine ya utalii wa mikutano ya kimataifa.

“Ni asilimia 20 tu ya fursa za utalii zilizopo Tanzania ndizo zinatumika licha ya kuwa na fursa kibao katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” alisema.

Prof. Mkenda alisema maonyesha ya kimataifa ya utalii ya Karibu-Kili Fair ni moja ya mkakati na ubunifu wa kusaidia kuchochea na kutangaza vivutio vilivyoko Tanzania.

Alisema vipo vivutio vingi vya malikale katika kanda mbalimbali za utalii kuwa ni pamoja na Iringa, Rukwa, Songwe, Mwanza, Mtwara, Lindi, Kigoma na Kagera ambavyo havijatangazwa vya kutosha.

Alisema lengo la serikali ni kuongeza idadi ya watalii watakaokuja Tanzania kutoka milioni 1.3  hadi milioni 1.5

Prof. Mkenda alisema mikakati hiyo inafanyika pamoja na uboreshaji wa huduma mbalimbali za utalii kwa kuimarisha mafunzo katika vyuo vya utalii.

Habari Kubwa