NIT kuanzisha mafunzo taaluma ya reli

18Mar 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
NIT kuanzisha mafunzo taaluma ya reli

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) cha jijini Dar es Salaam, kinatarajia kuanzisha kozi za usafiri wa reli zitakazozalisha wahandisi mbalimbali wakiwamo wa kuhudumia mabehewa na wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano ya reli.

Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mganilwa.

Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mganilwa, aliyasema hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipofanya ziara chuoni hapo kujionea mikakati na masuala ya maendeleo.

Profesa Mganilwa alisema wakati huu serikali ikijenga miradi mikubwa kama reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR), ni vyema kwa NIT kuanza kuzalisha wataalamu watakaofanya kazi katika miradi hiyo.

Alisema NIT inatarajia kuanzisha kozi ya masuala ya reli kupata wataalamu watakaohusika na usafiri, kuhudumia mabehewa, teknolojia ya mawasiliano ya reli na wataalamu wa menejimenti ya reli.

Alisema kwa sasa serikali imepokea misaada miwili mikubwa kwa ajili ya kukisaidia chuo hicho, wa kwanza ni wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) wa Sh. bilioni 50 ambazo zitatumika kukijengea chuo uwezo wa kuzalisha wataalamu kuingia katika sekta ya anga.

Alisema utawezesha nchi kupata marubani, wahandisi wa kutengeneza ndege, pamoja na wahudumu ndani ya ndege kupitia kozi zitakazotolewa chuoni hapo.

Alisema mwingine ni msaada wa Sh.bilioni 150 kutoka Serikali ya China, fedha zitakazosaidia NIT kuwa chuo kikuu cha usafirishaji na chuo cha kikanda.

“Mkopo huo utaanzisha ndaki (college) ya sayansi ya baharini kwenye chuo kitakachoanzishwa mkoani Lindi, ili kupata wataalamu wa kujenga na kutengeneza meli,” alisema Prof. Mganilwa.

Naibu Waziri anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alisema NIT ni mojawapo ya chuo kinachotegemewa na serikali katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya nchi.

Alisema wakati huu serikali ikijenga mradi mkubwa wa reli pamoja na ununuzi wa ndege, NIT inakuwa ni msaada mkubwa katika kukamilisha na kufikia malengo hayo.

“Kozi ya uhudumu wa reli na treni ikianzishwa itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa sababu wataalamu wengi wazawa watapatikana,” alisema Nditiye.

Aidha, alisema serikali imekuwa ikikisaidia NIT katika kupata mikopo nafuu kutoka kwa wafadhili mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso, alisema kama chuo hicho kitawezeshwa katika uboreshaji miundombinu, watumishi na vitendea kazi, serikali itapata wataalamu wenye ujuzi kwenye sekta ya anga na usafirishaji.

Alisema uwezo wa NIT kwa sasa ni mkubwa licha ya kukabiliwa na uhaba wa watumishi na vitendea kazi ambavyo kama serikali itatatua tatizo hilo kuna uwezekano kikawa chuo tegemezi nchini.

Habari Kubwa