NMB kuwakopesha wachimbaji wadogo bil. 120/-

26Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
NMB kuwakopesha wachimbaji wadogo bil. 120/-

WACHIMBAJI wadogo wamepata fursa baada ya Benki ya NMB Plc kusema imepanga kutumia zaidi ya Sh. bilioni 120 kutoa mikopo ya mitaji, vifaa na mitambo kwa wachimbaji wa madini.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi, Robert Gabriel Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ‘ NMB Mining Club’ kwa Kanda ya Ziwa.

Lengo la mpango huo ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuongeza tija katika sekta ya madini nchini.

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa Klabu la Wachimba Madini Kanda ya Ziwa, Mkuu wa Idara ya Biashara kutoka makao makuu ya benki hiyo, Alex Mgeni, alisema hadi sasa benki imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.3 kwa kundi hilo.

“Wachimbaji wadogo watakopeshwa vifaa na mitambo bila kulazimika kuweka dhamana, kwa sababu mitambo na vifaa hivyo ndivyo vitakuwa dhamana yao baada ya kulipa kuanzia asilimia 20 ya thamani ya kifaa au mtambo anaotaka kununua,” alisema Mgeni.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyoshirikisha wachimbaji kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Geita, Shinyanga na Kagera, Rais wa Shirikisho la Wachimba Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, alisema uamuzi wa Benki ya NMB kuanzisha dirisha la mikopo kwa sekta ya madini siyo tu utaongeza tija, bali pia utakuza uchumi wa wachimbaji na Taifa kwa ujumla.

Sehemu ya wageni waalikwa ambao ni miongoni mwa wachimba madini wa Kanda ya Ziwa wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa NMB Mining Club uliofanyika katika hotel ya Gold Crest- Mwanza.

“Teknolojia na mitaji ni kati ya changamoto sugu katika sekta ya madini, hasa kwa wachimbaji wadogo; benki ya NMB kutoa mikopo kutamaliza tatizo la mitaji na pengine litamaliza pia suala la teknolojia kwa sababu wachimbaji wataweza kuajiri wataalamu na hatimaye kuchimba kwa tija,” alisema Bina.

Alizihakikishia taasisi za fedha fursa ya biashara ya mikopo katika sekta ya madini aliyosema yanaongezeka thamani hata katika kipindi hiki dunia inakabiliwa na janga la virusi vya corona.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, aliihakikishia NMB utayari wa serikali wa kushirikiana na taasisi za fedha na wadau wengine kutekeleza sera na mikakati ya kuongeza tija katika sekta ya madini aliyosema imekuwa kwa kasi ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi, Robert Gabriel, pamoja na  Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa NMB , Alex Mgeni wakifuhia jambo baada ya uzungumza rasmi wa Klabu ya Madini ya ‘NMB Mining Club’ kwa Kanda ya Ziwa, kushoto ni Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Dickson Richard na  Rais wa Shirikisho la wachimba Madini, John Bina.

“Mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umepanda kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka wa fedha wa 2019/20 na inatarajiwa kufika zaidi ya asilimia 10 ifikapo mwaka 2025. Serikali iko tayari kushirikiana na taasisi za fedha kuongeza tija katika sekta ya madini,” alisema Gabriel.

Aliwashauri wachimbaji wadogo kuunganisha nguvu kimtaji kumudu siyo tu kufungua migodi ya kati na mikubwa, bali pia kutoa huduma katika migodi mikubwa ya kimataifa kupitia sera ya local content inayoelekeza sehemu ya huduma migodini kutolewa na kampuni za wazawa.