Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Foundation, Ruth Zaipuna, alisema wameanza kupokea maombi kupitia matawi yote ya benki hiyo yaliyoko nchi nzima na tovuti ya NMB Foundation.
“Kwa kuanzia tutatoa ufadhili kwa wanafunzi 200, ambapo 150 watakuwa wa kidato cha tano na sita, wanafunzi 50 watakuwa wa elimu ya juu. Ufadhili utalipia gharama zote za masomo ikiwamo ada, fedha za kujikimu, vifaa na mahitaji mengine yatakayotajwa kwenye fomu ya kujiunga na shule au chuo,” alisema Ruth.
Alifafanua kuwa kwa wanafunzi wa sekondari watakaopata ufadhili watalipiwa ada, nauli, vifaa vya kujifunzia, fedha za kujikimu, bima ya afya na mahitaji mengine watakayotakiwa kutoka shule. Kwa upande wa elimu ya juu, wanafunzi watalipwa ada, fedha za kujikimu, fedha za mafunzo kwa vitendo, Laptop na gharama nyingine watakazotakiwa kwenye fomu ya kujiunga na chuo.
Aidha, Zaipuna alisema wamejipanga kuweka masomo ya vipaumbele kwa wanafunzi watakaopata fursa ya udhamini. Lengo ni kuhakikisha wanashiriki mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kupitia malezi na mafunzo watakayopata wanafunzi hao.
“Tutaangalia kwa kina masomo ya takwimu na mahesabu, biashara na uchumi, teknolojia ya mawasiliano ya umma, uhandisi, mafuta na gesi pamoja na sayansi na teknolojia,” alibainisha Zaipuna na kuongeza:
“Nina imani kupitia programu hii tutaibua vipaji na tutatimiza ndoto za vijana. Kadiri tutakavyoendelea idadi ya wanafunzi watakaonufaika itaongezeka kulingana na mahitaji ambapo tutapanua wigo wa wadau wengine watakaotaka kushirikiana nasi kwenye jambo hili muhimu kwa maendeleo ya nchi.”
Katika hatua nyingine, Ruth alisema NMB Foundation itahakikisha watu watakaohusika kukusanya na kupitisha wanafunzi wanaofaa kwa kupewa ufadhili watakuwa makini kutimiza vigezo, ambapo kwa wale watakaokwenda kinyume na utaratibu watachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Tunataka kulifanya zoezi hili liwe na uwazi na ukweli, ndio maana tumesema tutawashirikisha hata viongozi wa serikali za mitaa kuanzia kata hadi mitaa, lengo ni kuhakikisha wanufaika watakaopatikana ni kweli wana vigezo vinavyohitajika,” alisisitiza Zaipuna.