NMB sasa yachangamkia ujio watalii

15May 2019
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
NMB sasa yachangamkia ujio watalii

WAKATI watalii 343 kutoka nchini China, wakiendelea na ziara yao ya siku tano katika baadhi ya Hifadhi za Taifa nchini pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Benki ya NMB imejitwisha jukumu la kupeleka huduma za kubadili fedha za kigeni katika kila eneo wanakapofika watalii hao.

Taarifa iliyopatikana jana na kuthibitishwa na Meneja wa NMB anayeshughulikia Dawati la China, Agness Mulolele ilieleza kuwa lengo la kusogeza huduma hiyo kwa Wachina hao ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuendelea na kukuza utalii nchini.

“Ni kweli tumeamua kusogeza huduma karibu ili kuweza kuwahudumia watalii wote katika huduma zote za kifedha. Huduma hiyo ya kubadili fedha za kigeni itawahusu zaidi wafanyabiashara na watu maarufu, wawekezaji kutoka kampuni 27, waandishi wa habari 40, maofisa wa serikali ya China na mawakala wa kampuni za utalii waliokuja kutembelea vivutio mbalimbali vya utali,” alisema Mulolele

Alisema wameamua kwenda kutoa huduma zao kama sehemu ya kusaidia nchi kufikia malengo makubwa ya maendeleo ikiwemo kuweka mazingira bora kwa watalii wanapotembelea nchini ili waweze kupata huduma bora za kibenki ikiwemo kubadirisha fedha za kigeni.

Juzi, Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa, akizungumza na watalii hao baada ya kuwapokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alisema Tanzania na China ni nchi zenye historia ndefu na ni marafiki wa siku nyingi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watalii hao, alisema bado Tanzania itazidi kufanya mambo makubwa hasa katika sekita ya utalii.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema, “Labda niseme kuwa sasa serikali imeanza kutuelewa sisi watu wa sekta ya utalii maana mbali na wageni hawa ambao ni zaidi ya 300, bado muda si mrefu tutapokea watalii tena 1000 lakini pia mwishoni mwa mwaka huu tutakwenda Russia kwa masuala ya utalii. Kwa hiyo naomba nitoe wito pia Watanzania kuwa ni muda sasa wa kujifunza lugha tofauti tofauti ili iwe fursa nzuri ya kujipatia ajira.”

Aidha, alisema dhamira ya Bodi hiyo ya Utalii nchini ni kutangaza utalii katika soko la China na kwamba Juni mwaka huu, wanatarajia kufanya ziara ya kutangaza utalii katika miji ya Nanjing, Hanzhou na Changsha,”

Habari Kubwa