NMB yaendelee kuwa kinara wa huduma mara tisa mfululizo

03Aug 2021
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB yaendelee kuwa kinara wa huduma mara tisa mfululizo

Benki ya NMB imeendelea kuwa kinara, baada ya kupata tuzo mbili za umahiri za Euromoney kutoka majarida mawili makubwa ya kimataifa kwa mwaka 2021 hiyo ikiwa ni mara ya tisa (9) mfululizo kutambulika kama benki bora zaidi Tanzania.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akimkabidhi Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. George Mulamula, Tuzo ya umahiri ya Euromoney kama Benki Bora Tanzania 2021 na Benki bora huduma kwa wateja binafsi na Biashara wakati wa hafla iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya tuzo hizo leo Agosti 03,2021 Dar es salama, Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna amesema tuzo hizo ni heshima kubwa na kielelezo tosha kuwa benki inazidi kujijenga katika sekta ya kibenki.

Amesema kuwa tuzo hizo zimetolewa na jaridi maarufu la Jijini London linaloitwa Global Banking and Finance ambalo kwa kuitambua benki ya NMB kuwa bora zaidi Tanzania kwa huduma za wateja binafsi na biashara za kati kwa mwaka 2021.

Amesema tuzo hiyo ni tuzo ya juu kabisa inayotolewa na majarida makubwa Duniani  yanayoaminika katika kufanya tafiti za taasisi za kifedha na kutambua mchango wao katika kuboresha huduma za kibenki.

Hata hivyo amesema ubunifu uliopo ndani ya benki ya NMB, uwekezaji katika Teknolojia, suluhisho za kidigitali pamoja na mtandao mpana wa matawi, mawakala na mashine za kutolea fedha vimechangia katika kuleta mabadiliko makubwa ndani ya benki na kuifanya kuwa benki bora zaidi hapa nchini.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya benki ya NMB Dk. George Mulamula amewashukuru wateja na watanzania wote kwa kuifikisha benki ya NMB hapo ilipo wajibu wao ni kuhakikisha wanaendelea kufanya vyema na kuendelea kuwa benki bora inayoakisi kasi ya serikali.

Dk. Mulamula ametoa rai kwa Menejimenti na wafanyakazi wa benki ya NMB kutobweteka na ushindi huo na kuongeza utendaji na ufanisi ili kukuza zaidi utendaji na ubora wa benki ya NMB.

Tuzo zote mbili zimetolewa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyopendekezwa ikiwemo ufanisi wa utendaji, huduma za kidijitali, huduma jumuisha za kifedha, usalama wa huduma za kimtandao na uwajibikaji wa benki katika jamii, mtaji wa benki, mapato yatokanayo na mali za benki na yasiyotokana nariba pamoja na kiwango cha mikopo, uwiano na amana za wateja.