NMB yasisitiza miundombinu bora

08Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
NMB yasisitiza miundombinu bora

WAJUMBE wa Benki ya NMB wameuomba uongozi wa serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja kuandaa miundombinu rafiki ili kufikia maendeleo ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Meneja wa NMB Tawi la Zanzibar, Duchi Amour Duchi , alisema hayo jana walipofanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja na viongozi na watendaji kwa lengo la kujadili namna ya kuwasaidia vijana na kinamama wa kutumia fursa mbalimbali ziliko ndani ya mkoa huo hususan ujasiriamali na ushirika.

Alisema mkoa huo una fursa mbalimbali kutokana na mazingira ya kijiografia zikiwamo kilimo, uvuvi na utalii ambazo zinaweza kuwakomboa kiuchumi wananchi huku akiahidi kutoa mafunzo katika sekta hizo.

Alisema mafunzo hayo yatalenga namna ya kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika soko ili kupatikana na kuzalishwa kwa wingi na kuulinda mtaji ili uendelee kukua zaidi wakipatiwa mikopo.

"Mkoa huu wa Kusini umebarikiwa kuwa na shughuli nyingi za ujasiriamali ambazo kinamama wakipatiwa mitaji basi watapiga hatua za kimaendeleo, mfano kuna sekta ya kilimo, uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupitia vikundi vya ushirika, uvuvi, kilimo cha mwani na hata shughuli za ufugaji kwa hiyo ipo haja ya kupatiwa mafunzo ili bidhaa zao zizalishe katika kiwango kinachotakiwa," alisema.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema sasa wakati umefika kwa wananchi wa mkoa huo kuwa na mradi wa ufugaji kuku kwa wingi ili kuweza kuwapeleka hotelini na kuachana na kuagiza kutoka soko la mjini.

Alisema kuwapo kwa machinjio ya kisasa ya kuku kila wilaya za mkoa huo zitasaidia zaidi kukuza biashara ya ufugaji wa kuku na kupelekea kufikia soko uhakika na kuongeza kipato cha wananchi.

Mkuu wa Mkoa amewataka wakuu wa wilaya kuweza kutumia fursa hiyo ya ujio wa NMB kuweza kuandaa vikao vya pamoja ambavyo vitaleta tija kwa serekali na wananchi wa mkoa huo.

Nao wakuu wa wilaya mbili za Mkoa huao ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini wameuomba ujumbe huo kuweza kusaidia mabaraza ya vijana na vikundi vya ushirika ili kuweza kuvipeleka mbele kimaendeleo kwani kufanya hivyo kutapanua wigo wa kibiashara kati ya NMB na wananchi wa mkoa huo.

Ujumbe huo wa NMB uliokwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Ungunja ni Meneja Uhusiano Idara ya biashara za Serikali za kibenki, Mkunde Joseph na Meneja Idara ya Biashara na Kilimo NMB, Makao Makuu, John Machunda.

Habari Kubwa