NMB yazindua Bonge la Mpango; kujishindia hadi Sh. mil 500

23Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB yazindua Bonge la Mpango; kujishindia hadi Sh. mil 500

BENKI ya NMB imezindua kampeni inayojulikana kama ‘Bonge la Mpango’ ambayo itawawezesha wateja kushinda fedha taslimu, pikipiki ya miguu mitatu, gari aina ya Tata - Kirikuu na gari ya kifahari aina ya Toyota Fortuner.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi akionesha aina ya gari - Toyota Fortune mpya inayoshindaniwa katika Bonge la Mpango. Wengine ni baadhi ya viongozi wa Benki ya NMB

Katika kampeni hiyo zaidi ya Sh. milioni 550 zitatumika kutoa zawadi kwa washindi, huu ukiwa ni mkakati wa benki hiyo kwa mwaka 2021 unaokusudia kuendelea kuifanya kuwa chaguo la kwanza kwa wateja kwa usalama wa fedha zao pamoja na uhakika wa huduma nyingine za kibenki.

Wateja wote wa NMB wanaofika zaidi ya Milioni 3 nchini wana nafasi ya kushinda zawadi wakati mshindi wa mwisho atajinyakulia Toyota Fortuner mpya (kilomita 0 ) yenye thamani ya Shilingi milioni 169.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi alisema ni hii ni moja ya njia za kurudisha faida kwa wateja wao waaminifu wanaotunza fedha ndani ya benki hiyo huku ikikusudia kuhamasisha utamaduni wa kutunza akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye."

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, akizindua rasmi kampeni ya Bonge la Mpango inayowazawadia wateja pesa taslimu, pikipiki za miguu mitatu , gari ya mizigo alimarufu Kilikuu na Toyota Fortune mpya. Wakishangilia ni baadhi ya  viongozi wa Benki ya NMB.

"Wateja wanaoweka akiba ya walau Sh. 100,000 wataingia kwenye orodha ya wanaostahili zawadi zilizopo ambazo ni fedha taslimu Sh. 500,000 kwa washindi 10 kila wiki, pikipiki ya kubebea mizigo aina ya LIFAN, Gari ya kubebea mizigo maarufu kama Kirikuu au Toyota Fortuner, kampeni hii itaendelea mpaka Mwezi Mei mwaka huu," alisema Mponzi na kuongeza kuwa;

“Tunatoa fursa kwa wateja wetu sambamba na kuwahamasisha kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba hasa kipindi hiki ambacho kila mmoja anaugulia maumivu ya msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka uliomaliza fedha,” 

Kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha wasio na akaunti ya benki nchini kufungua na kutunza akiba zao kwa njia salama zaidi na benki ya NMB, hiyo ni kwa kuwa benki hiyo inaongeza, "NMB Inakusudia kuhamasisha utamaduni wa kujiwekea akiba, umuhimu na thamani ya kampeni hii utathibitisha jinsi benki hiyo inavyowajali wateja wake bila kuwasahau wananchi wasiotumia huduma za benki,"

Aina tatu za zawadi zinazoshindaniwa ndani ya Bonge la Mpango; Pikipiki za miguu mitatu , gari ya mizigo alimarufu Kirikuu na Toyota Fortune mpya.

Alifafanua kuwa ili kukidhi vigezo na sifa za kujishindia zawadi zitakazotolewa, mteja anatakiwa kuweka akiba kwenye akaunti yake, pia  mteja atakayefungua akaunti na kuweka akiba ya Sh. 100,000 au zaidi iwe kwa fedha taslimu au kuhamishia kwenda akaunti yake ya Benki ya NMB anajiweka kwenye nafasi ya kushinda zawadi zitakazotolewa kila wiki na atakuwa sehemu ya watakaoshindania zawadi ya mwezi itakayotoa washindi watatu wa gari ya mizigo - "Kilikuu" au pikipiki ya mizigo aina ya LIFAN.

Droo ya mwisho itawahusisha wateja ambao wana akiba ya zaidi ya Sh. milioni 10 kwenye akaunti zao iliyodumu kwa zaidi ya siku 30,wateja hao wanaweza kujishindia gari aina ya Toyota Fortuner yenye thamani ya Sh. milioni 169.

Habari Kubwa