NSSF kusaka fedha za wavuvi

11Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
NSSF kusaka fedha za wavuvi

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umedhamiria kuwafikia wavuvi katika maeneo mbalimbali nchini, ili waweze kufaidika na mafao ambayo yamekuwa yakitolewa.

Hayo yalielezwa jijini Dodoma na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mfuko huo, Lulu Mengele, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mfuko huo.

Alisema kuwa lengo la mfuko huo ni kuhakikisha linawafikia watu wa makundi mbalimbali katika jamii zote ili waweze kunufaika na huduma ambazo wamekuwa wakizitoa zitakazo wasaidia kuwakinga katika majanga mbalimbali.

Mengele alisema kuwa sababu za kuanzisha mpango wa hifadhi ya jamii kwa wavuvi umekuja baada ya kubaini kuwa wengi wao wanazo sifa za kujiunga na mpango huo, lakini walikuwa hawajui faida zake na hivyo kukosa mambo muhimu wao na familia zao.

"Wavuvi wengi wanazo nafasi hizo, wanapata shida kubwa pindi wanapokumbana na majanga kama ya ajali katika bahari, maziwa wakati wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi wa samaki wanakumbana na changamoto mbalimbali," alisema Mengele.

Aidha, alisema kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 44, ambapo milioni 4.5 wanajishughulisha na uvuvi, lakini walikuwa hawajafikiwa na mpango wa hifadhi ya jamii, tofauti na ilivyo sasa.

Aliyataja baadhi ya mafao ambayo wavuvi watafaidika nayo kuwa ni pamoja na fao la kuwakiga na majanga, fao la matibabu, fao la mikopo ya riba nafuu kwa ajili kununulia pembejeo, kusomesha watoto wao na shughuli zingine za maendeleo.

Alisema kuwa mpango huo utasaidia serikali kupunguza umaskini kwa jamii, kujenga kizazi kisichokuwa tegemezi kwa kutoa pensheni ya ya uzee, urithi na ulemavu pamoja na kupambana na umaskini kwa ujumla.