Ombi vikundi vya uzalishaji

01Jan 2018
Renatha Msungu
Nipashe
Ombi vikundi vya uzalishaji

SERIKALI imetakiwa kuangalia namna ya kuviongezea nguvu vikundi vya kuzalisha mkaa mbadala utokanao na mabaki ya mazao na takataka, ili kuokoa misitu nchini.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini hapa na Mkurugenzi wa Tools Manufactures, Leonard Kushoka, wakati wa kikao cha pamoja cha kujadili changamoto ya utegemezi mkubwa wa nishati ya mkaa na tishio la kutoweka kwa misitu Tanzania.

 

Alisema misitu ya Tanzania inateketea kwa kiwango kikubwa na ipo haja ya vikundi kuwezeshwa katika maeneo mbalimbali nchini, ili kutengeneza mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya mazao na takataka ili kuokoa misitu.

Alisema akiwa ni mbunifu wa mashine ya kutengeneza mkaa mbadala yuko tayari kushirikiana na serikali kusambaza mashine hizo.

 

“Lazima kutengeneza biashara pinzani ya mkaa ndani ya miji kama tunataka kuokoa misitu,” alisema.

 

“Kwa sasa tunajishughulisha na utengenezaji mashine za kuzalisha mkaa mbadala na kuzisambaza kwa jamii tukiwa tumeanza na jiji la Dar es laam, Mwanza, Arusha na sehemu mbalimbali nchini,” alisema.

 

Alisema mashine wanazotengeneza zina uwezo mkubwa wa kupunguza au kumaliza tatizo hili kwani mashine moja ina uwezo wa kuzalisha hadikilogramu 1500 za mkaa mbadala kwa siku ikitumia malighafi isiyozidi kilogramu 3,250 ambazo ni takataka au mabaki ya mazao.

“Mashine hizi ni fursa ya uchumi kwa jamii pia chanzo cha kuweka mazingira safi na salama kwa asilimia 60 ya takataka zinazozalishwa mijini ni malighafi ya kuzalisha mkaa,” alisema.

“Tunataka serikali kuiona fursa hii ya kuanzisha viwanda vidogo vingi vya kuzalisha mkaa mbadala na kuipatia nafasi inayostahili kwani ukizalisha mkaa ndani ya miji utaua soko la mkaa wa kutoka msituni,” alisema.

Alisema mkaa huu ni rafiki kwa jamii kwani utapatikana katika vipimo vilivyozoeleka kuanzia Sh. 500 kwa kilo moja.

“Kwa sasa tunatengeneza mashine kwa wingi na kuziuza kwa bei nafuu kwa jamii pia tunawafundisha jinsi ya kuzalisha mkaa mbadala,” alisema.

Alisema kauli za viongozi wa kisiasa hazipaswi kurudi nyuma kwani kuna wakati kuna marufuku za kuzuia mikaa isiingizwe mijini na marufuku hizo zimekuwa zikifutwa baada ya kutolewa.