Onyo mamlaka maji ubambikaji wa bili

14Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Onyo mamlaka maji ubambikaji wa bili

MAMLAKA za maji nchini zimetakiwa kutowabambikia bili kubwa za huduma hiyo wateja wake na zitakazobainika zitachukuliwa hatua kali.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, alitoa onyo hilo bungeni mjini hapa jana alipokuwa anajibu swali la Seif Gulamali.

Akiuliza swali la nyongeza, mbunge huyo wa Manonga (CCM), aliitaka serikali kutoa kauli kuhusu kadhia hiyo baada ya awali kuiuliza serikali itabadili lini mita zote za maji nchini, ili wananchi wanunue kwa mfumo wa uniti kama ilivyo kwa umeme kwa kuwa sasa wanabambikiwa bili kubwa kuliko matumizi.

Katika majibu yake, Aweso alikiri kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuongezwa bili za maji kuliko matumizi yao halisi.
Naibu Waziri huyo alisema hilo ni kosa na atakayebainika, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

"Tukibaini mamlaka yoyote ikifanya vitendo hivyo hata kama ana mapembe makubwa kiasi gani, tutayakata ili wananchi wetu wapate maji na walipe kinachostahili," alisema.

Kuhusu kulipa kwa uniti, Aweso alisema wizara yake imeanza kuufanyia kazi mfumo huo na sasa uko katika majaribio ya mfumo wa malipo katika baadhi ya halmashauri kabla ya kuanza kutoa huduma hiyo nchi nzima.

Alisema kwa kupitia mfumo huo, mteja hufungiwa kifaa maalum kinachomwezesha kulipa kwanza kiasi cha maji anachohitaji kabla ya kutumia.

Aweso alisema kuwa hadi kufikia Oktoba mwaka huu, jumla ya mamlaka za maji saba zilikuwa zimeanza kuutumia mfumo huo kwa wateja wao.

Alizitaka mamlaka hizo kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Maji Iringa, Arusha, Dodoma, Mbeya, Songea, Tanga na Dar es Salaam (Dawasco).

Alisema kwa sasa mfumo umeonyesha mafanikio makubwa na kwamba kuwa kutokana na ukubwa wa gharama za mfumo, wizara imeziagiza mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira daraja A kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya kuendelea kufunga mfumo huo.