Operesheni uvuvi haramu yazaa matunda 

10Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
MWANGA
Nipashe
Operesheni uvuvi haramu yazaa matunda 

ZAIDI ya mitumbwi 240, ndoo 84 zenye samaki zimekamatwa  na kokoro 44  zimesalimishwa  katika Operesheni ya Kukamata Uvuvi Haramu...........

Unaendelea katika Bwawa la Nyumba ya Mungu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kulifunga Bwawa hilo kwa muda wa mwaka mmoja

Akitoa taarifa ya Kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Enea Mrutu, alisema kukamatwa kwa mitumbwi na ndoo hizo za samaki kumetokana na utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alilolitoa kuhusu kutokuruhusu shuhuli zozote za uvuvi katika bwawa hilo.

Mrutu alisema mapambano dhidi ya uvuvi haramu yanapaswa kuungwa mkono na kila mtumishi wa umma na wananchi kushirikiana na watumishi wanaoendesha operesheni hiyo kwa kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa wavuvi hao.

"Waheshimiwa madiwani, hili bwawa ni letu na tunapaswa kuwaeleza wananchi kutoa ushirikiano katika kuwafichua wavuvi ambao wanaingia bwawani na kuvua samaki ambao ni wadogo. ni wakati wa madiwani kumuunga mkono mkuu wetu wa mkoa ili kusaidia samaki waendelee kukua," alisema Mrutu

"Hadi sasa haijulikani ni ngalawa ngapi zilizosajiliwa kufanya shughuli zake bwawani. Kamati inaiomba halmashauri kupitia wataalamu wake kusajili ngalawa zote ili pia kuongeza mapato ndani ya halmashauri," alisema.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa kesi saba zimefikishwa mahakanani na pikipiki  mbili zimekamatwa huku akiongeza kuwa gari moja lilikamatwa na kutozwa faini na kuachiwa.

"Hadi sasa ngalawa 249 zimesajiliwa lakini utafiti wa kamati unaonyesha kuwa kuna zaidi ya ngalawa 500 na hazijasajiliwa,tunaiagiza idara husika kutimiza wajibu wao pindi bwawa litakapofunguliwa kusajili ngalawa zote zilizopo na ambazo hazitasajiliwa zikamatwe," alisema.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo, Theresia Msuya, aliwataka madiwani wa halmashauri hiyo kuchapa kazi na kuacha kulalamika huku akimwagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kutoa usafiri kwa watumishi watakaohusika kwenye operesheni za kuwakamata wavuvi haramu.

Pia alisema umefika wakati wanatamani kufanya kazi na mgambo kwa kuwa  wanapofanya kazi  nao wanafanikiwa kulinganisha na askari ambao huwa hawafanikiwi kutokana na kuonekana kuwa na mtandao wa watu hao.

Katika hatua nyingine, Diwani wa Kigonigoni, Jeremia Shayo, alitaka kujua ni lini halmashauri hiyo itarudisha asilimia 20 ya mapato ya ndani kwenye vijiji ili vijiendeshe. 

"Mwenyekiti, halmashauri yetu ina vijiji 72, asilimia kubwa ya vijiji vyetu havina ofisi.  Inashangaza sana kwani vijiji hivyo hivyo vinawasilisha mapato halmashauri lakini hawapewi asilimia zao 20 kama sheria inavyoeleza.

Pia  baadhi ya vijiji havina ofisi na mapato yanakusanywa," alisema Shayo.

Akijibu swali hilo, Msuya alisema hiyo inatokana na akaunti nyingi za vijiji kutokufanya kazi ikiwa ni pamoja na nyingi kufa huku  akizitaka halmashauri hizo za vijiji kuzifufua mara moja.

Msuya aliongeza kuwa pamoja na kufufuliwa kwa akaunti hizo, ni vyema ikafahamika kuwa ruzuku ya uendeshaji kutoka serikali kuu inakuja kwa kusuasua huku akimtaka mkurugenzi kuwapa fedha halmashauri zote za vijiji zilizokidhi kupewa asilimia 20 ya fedha zao za mapato.

Habari Kubwa