Operesheni ya uvuvi haramu yaingiza bil. 2/-

03Dec 2018
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Operesheni ya uvuvi haramu yaingiza bil. 2/-

OPERESHENI za kudhibiti uvuvi haramu nchini zimewezesha serikali kupata Sh. bilioni 2.29 katika kipindi cha kuanzia Desemba 2017 hadi Novemba mwaka huu.

Hayo yalibainishwa juzi na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alipoongoza kikao cha kufanya tathmini ya Operesheni Sangara awamu ya tatu iliyofanyika Kanda ya Ziwa Victoria.

Kikao hicho kilichofanyika jijini Mwanza, kilihudhuriwa na maofisa waliohusika katika operesheni hiyo.

Alisema kuwa mwaka 2016/17, Sh. milioni 457 zilipatikana kutokana na operesheni za uvuvi haramu na kwamba mwaka huu kuna ongezeko la makusanyo kufuatia udhibiti wa mianya ya utoroshaji fedha.

Katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na baadhi ya wafanyabiashara wa samaki, Ulega alisema kabla ya kuanza kwa operesheni za kudhibiti uvuvi haramu, takwimu zilionyesha uwapo wa samaki wachanga zaidi ya asilimia 90, lakini baada ya operesheni hizo samaki waliongezeka.

Akiwasilisha taarifa ya operesheni hiyo, Ofisa Mfawidhi wa Kanda hiyo, Didas Mtambalike, alisema tangu kuanza kwa operesheni hiyo Oktoba 18 hadi Desemba Mosi mwaka huu, Sh. bilioni 1.172 zilipatikana kutokana na malipo ya faini walizotozwa waliojihusisha na matukio ya uvuvi haramu.

Mtambalike alisema operesheni hiyo imewezesha vyombo vingi vya uvuvi na biashara za bidhaa za uvuvi kusajiliwa na kupatiwa leseni kutokana na elimu ambayo wavuvi walikuwa wakipatiwa ili kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

Baadhi ya wadau wa uvuvi ambao walipata nafasi ya kutoa maoni yao katika kikao hicho, waliiomba serikali kuhakikisha kunakuwapo na bei elekezi kwa mazao ya samaki ili wavuvi wauze samaki kwa bei ya uhakika. 

 

 

Habari Kubwa